ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 20, 2012

TFF 'yawafungulia' kina Cannavaro

Wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar waliofungiwa mwaka mmoja na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kucheza soka mahala popote kutokana na madai ya utovu wa nidhamu, hawatatumikia adhabu hiyo hadi Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakapokaa kujadili maamuzi hayo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah aliiambia NIPASHE jana kuwa wameiandikia barua ZFA kuifahamisha kwamba wamepokea barua ya chama hicho cha soka inayowafahamisha kuhusu kufungiwa kwa nyota hao, lakini wameipeleka katika Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF kwa hatua zaidi, hivyo kwa sasa shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo.   

"Tumewaandikia barua ZFA, tumewafahamisha kwamba tuko pamoja na nidhamu ni lazima ilindwe, lakini kwa sasa wachezaji hawatatumikia adhabu hiyo hadi baada ya kikao cha kamati ya nidhamu," alisema Osiah.

Kwa maana hiyo, Osiah alisema, wachezaji walio katika kambi ya timu ya taifa (Taifa Stars) wataendelea kuitumikia timu hiyo katika kambi ya kujiandaa kuwakabili mabingwa wa Afrika, Zambia 'Chipolopolo' katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Baadhi ya wachezaji hao ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Aggrey Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis, Mwadini Ali, Seif Abdallah na Selemani Kassim 'Selembe'.

Kamati ya Utendaji ya ZFA ilifanya maamuzi ambayo yalipaswa kufanywa na Kamati ya Nidhamu ya chama hicho ya kuwafungia wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa kitendo chao cha kuamua kugawana zawadi ya Dola 10,000 walizopata baada ya kushinda nafasi ya tatu ya mashindano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) 2012 baada ya kuwafunga ndugu zao wa Tanzania Bara kwa penalti 6-5 mwezi uliopita nchini Uganda.

ZFA pia iliilalamikia TFF kwamba shirikisho hilo la soka nchini limepuuza adhabu iliyotolewa na chama hicho cha soka kwa "kuwaachia" wachezaji hao waendelee kujifua katika kambi ya Taifa Stars ilhali "wamefungiwa kucheza soka ndani na nje ya nchi kwa klabu na timu za taifa".  

Maamuzi ya ZFA kuwafungia wachezaji hao kuchezea hata klabu zao zenye mikataba nao na zinazowalipa mishahara kwa kosa walilolitenda wakati wakiichezea timu ya taifa, yalizua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka nchini wakiona kwamba ni maamuzi ya hasira zaidi ya uhalisia wa mambo.

Nahodha wa timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto'o, alifungiwa miezi minane na chama cha soka cha nchi yake kuichezea timu hiyo ya taifa kutokana na mgogoro wa kimalipo wakati akiwatetea wachezaji wenzake, lakini chama hicho hakina mamlaka ya kumzuia kuichezea klabu yake ya Anzhi Makhachkala ya Urusi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: