NA THOBIAS MWANAKATWE.
Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha umechukua sura mpya baada ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya hiyo kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kwa maelezo kwamba, haina mamlaka hayo.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Thomas Moshi Darabe, alisema kupitia taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana kuwa wamesikitishwa na uamuzi wa Kamati Kuu wa kuisimamisha kamati hiyo yenye wajumbe 17 bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza.
Alisema uamuzi huo wa Kamati Kuu unakiuka katiba ya Chadema ibara ya 6.5.6 na ibara 7.4.7 (g) inayoeleza kuwa kikatiba chombo chenye mamlaka ya kusimamisha/kuondoa Kamati ya Utendaji ya Wilaya ni Mkutano Mkuu wa chama wilaya.
Darabe alisema kwa burasa ya kawaida hata kama kulikuwa na sababu za kufanya hivyo, wangepewa hati ya kuitwa na kwamba, kwa maelezo hayo kamati ya utendaji ya chama wilayani humo iko kazini itaendelea na shughuli zake za kila siku.
Alisema awali, Kamati ya Utendaji Wilaya ya Karatu, ndiyo ilikuwa inawatuhumu baadhi ya viongozi kwa kudhoofisha chama na kushauri wachukuliwe hatua, lakini wakashangaa wanasimamishwa wao uongozi.
Darabe alisema kutokana na uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu, Kamati ya Utendaji ya Wilaya, madiwani wa Chadema na wadau wa chama hicho watafanya mkutano kuanzia kesho na keshokutwa.
Alisema mkutano huo utafuatiwa na mkutano wa hadhara wa wananchi utakaofanyika Jumamosi wiki hii, Karatu, ambao utahudhuriwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.
Mapema katika mkutano wake wa siku mbili mfululizo, uliohitimishwa Desemba 16, mwaka huu, Kamati Kuu ya Chadema ilifikia uamuzi wa kusimamisha uongozi wa chama hicho wilaya hiyo, baada ya kubaini kasoro za utendaji wa viongozi wake.
No comments:
Post a Comment