ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 16, 2012

Wachezaji Simba wampinga kocha mpya



Baadhi ya wachezaji wa Simba wamepinga maamuzi ya uongozi wa klabu ya kuvunja mkataba na kocha wa timu hiyo, Mserbia Milovan Cirkovic.

Wakizungumza kwa nyakatat tofauti na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao gazetini mwishoni mwa wiki, wachezaji wa Simba walisema Cirkovic alikuwa na uwezo mkubwa na pia alikuwa akielewana na wachezaji wake.



"Ni maamuzi ya uongozi," alisema mchezaji mmoja na kueleza zaidi, "lakini mimi naona kama maamuzi yao yatatuyumbisha kwa sababu kocha mpya hatakuwa na muda mrefu kuwasoma na kuwalewa wachezaji (kabla ya mzunguko wa duru la pili la ligi kuu ya Bara kuanza).

"Lakini ndio maamuzi ya viongozi na sisi tunabaki kuwa wachezaji tu."

Mchezaji mwibngine alisema hawataki kuuulaumu uongozi kwa kuwa wao ndio wanaojua sababu za kumwacha Cirkovic, lakini akasisitiza kuwa wachezaji hawakuwa na matatizo na kocha huyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Afisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema uongozi wa Simba umesitisha mkataba na kocha huyo kwa sababu kuu mbili:

Kwanza, kwasababu Simba haina uwezo wa kuendelea kumlipa kocha huyo hasa kutokana na mktaba wake kuwa wa gharama kubwa.

"Lakini si hivyo tu, pia uongozi umeona Milovan (Cirkovic) hashauriki na hataki kubadilika hasa juu ya aina ya mchezo ambao Simba wanacheza hasa wakiwa nje ya Dar es Salaam," alisema Kamwaga.

Naodha wa klabu hiyo, Juma Kaseja ambaye yupo na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, alisema jana kuwa hana cha kuzungumza juu ya uamuzi huo wa kuondolewa kwa kocha kwa kuwa ni maamuzi ya uongozi.

"Mimi sina cha kuongea," alisema Kaseja. "Kwanza nipo kwenye majukumu ya timu ya taifa hivyo siwezi kuzungumzia masuala ya Simba kwa sasa."

Simba imetangaza kumchukua kocha Mfaransa Patrick Liewig kwa ajili ya kuziba nafasi ya Cirkovic na kwamba atawasili mwishoni mwa mwezi huu.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: