Wednesday, December 26, 2012

Watoto 160 wazaliwa mkesha wa Krismasi

Baadhi ya akina mama waliojifungua watoto wakati wa mkesha wa Krismasi katika Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam. Kushoto alijitambulisha kwa jina moja la Elita na kulia hakutaka kutaja jina lake.

Watoto 160 wamezaliwa usiku wa mkesha wa Krismasi katika hospitali tofauti nchini. Kati yao, watoto 62 walizaliwa katika Hospitali ya Amana, iliyopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Muuguzi wa zamu wa hospitali hiyo, Pendo Sikaponda, alililiambia NIPASHE jana kuwa watoto wote walizaliwa salama na wanaendelea vizuri.

Alisema kati ya watoto hao, 30 ni wa kike na 32 ni wa kiume.

“Tunamshukuru Mungu. Watoto wote wamezaliwa salama, wakiwamo sita walizaliwa kwa njia ya upasuaji,” alisema Sikaponda.
Pia watoto 10 walizaliwa katika Hospitali ya St. Joseph Mission, iliyopo Peramiho, Wilaya ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma.

Sista Matilda Mkulu alisema kati ya watoto hao, wanane ni wa kike na wawili wa kiume na kwamba, wote 10 walizaliwa kwa njia ya kawaida.

“…Hakuna mtoto aliyezaliwa kwa njia ya upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri pamoja,” alisema Sista Mkulu na kuongeza kuwa mama wa watoto hao walipewa zawadi ya sabuni za kufulia nguo.

Vilevile, watoto watatu walizaliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam; mmoja akiwa ni wa kike na wawili wa kiume.

Kadhalika, watoto 25 walizaliwa katika Hospitali ya Mwananyamala, iliyoko Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam; 10 wakiwa ni wa kike na 15 wa kiume na wote wanaendelea vizuri baada ya kuzaliwa.

Pia watoto 53 walizaliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam. Muuguzi wa zamu, Asha Kitumbuizi, alisema mama wa watoto wote waliojifungua wanaendelea vizuri. Alisema kina mama waliojifungua kwa njia ya upasuaji ni wachache, lakini idadi kamili bado haijajulikana.

Pia watoto saba walizaliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

Imeandaliwa na Rehema Kilagwa, Adela Josephat, Zuhura Masudi, Jacqueline Yeuda, Sharifa Marira, Dar; Friday Simbaya, Songea na Mwandishi wetu, Bunda
CHANZO: NIPASHE

No comments: