Kikosi cha mwaka 1974 kikiwa kwenye Uwanja wa Maracana, Brazil
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC, mabingwa mara tano wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame wanatarajiwa kuondoka nchini saa 10:30 usiku wa kuamkia kesho nchini kwenda Uturuki kuweka kambi ya mazoezi ya wiki mbili.
Kikosi kizima cha Yanga kitakuwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kuanzia saa 8:00 usiku kwa taratibu za kusafiri katika ziara hiyo ya kwanza nje ya Afrika tangu walipokwenda Brazil mwaka 1974.
Yanga itaweka kambi katika mji wa Antalya uliopo kusini mwa Uturuki na itafikia katika hoteli ya Sueno Beach iliyopo pembezoni mwa bahari ya Meditreanian, na itakua ikifanya mazoezi katika viwanja vikubwa viwili vilivyopo katika hotel hiyo na kiwanja kidogo cha nyasi bandia.
Kikosi cha Yanga kinachoondoka leo ni makipa; Ally Mustafa 'Barthez', Said Mohamed na Yussuf Abdul, mabeki Juma Abdul, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ladisalus Mbogo na Kelvin Yondani.
Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Kabange Twite, Nurdin Bakari, Omega Seme, Simon Msuva, Rehani Kibingu, Nizar Khalfani na David Luhende wakati washambuliaji ni Didier Kavumbagu, Said Bahanunzi, Jerry Tegete, George Banda na Hamisi Kiiza.
Upande wa benchi la ufundi ni Kocha Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts, Kocha Msaidizi Freddy Felix Minziro na Kocha wa makipa, Razak Ssiwa, na Maofisa wengine ni Daktari wa timu, Sufiani Juma, Meneja Hafidh Saleh, Ofisa Habari, Baraka Kizuguto Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mohammed Nyenge.
Mwandishi wa Gazeti la Mwanaspoti, Michael Momburi atakuwapo kwenye ziara hiyo ya kwanza ya Yanga Ulaya, yeye akigharamiwa na kampuni yake.
Ziara ya mwisho katika nchi ya maana kwa Yanga, ilikuwa mwaka 2008 nchini Afrika Kusini, ambako iliweka kambi ya zaidi ya wiki mbili wakati huo ikiwa chini ya Profesa Dusan Savo Kondic, raia wa Serbia.
Zaidi ya hapo, mwaka huu Yanga ilikwenda Kigali, Rwanda kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara, kwa mwaliko wa rais wa nchi hiyo, Paul Kagame.
Yanga SC ni klabu kongwe Tanzania ambayo kati ya zinazoshiriki Ligi Kuu kwa sasa, yenyewe ndio yenye umri mkubwa zaidi.
Ingawa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.
No comments:
Post a Comment