Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, alisema kazi ya kuwachunguza maofisa hao iliyokuwa ikifanywa, imekamilika na wamepewa ripoti inayoonyesha kuwa kuna kasoro hasa katika ununuzi usiyofuata taratibu na ubadilishaji wa fedha za kigeni (Dola). Alisema kwa sasa bodi ipo katika mchakato wa kuunda jopo la watu sita litakalowaita maofisa hao na kuwahoji na kwamba kila mmoja atatakiwa kujibu tuhuma zinazomkabili.
Maofisa hao ambao wanasubiri uamuzi wa Bodi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi Harun Mattambo.
“Awali CAG alileta taarifa ambayo tuliikataa na kumtaka airekebishe. Hii ya mara ya pili tuliikubali na tumeielewa, kikubwa alichogundua ni ununuzi yusiyofuata taratibu na suala la kubadilishwa kwa Dola za Marekani katika benki ambazo Shirika halina akaunti,” alisema Mboma na kuongeza;“Benki ambayo Shirika halina akaunti na ambayo wangeweza kubalishia fedha hizo ni Benki Kuu (BOT) pekee, lakini haikufanyika hivyo jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu.”
Alisema baada ya jopo kumaliza kuwahoji watuhumiwa hao, litawasilisha mapendekezo kwa bodi ambayo itatoa uamuzi wake.
Maofisa hao walisimamishwa kazi Julai 14 mwaka jana sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, ambaye baadaye alifukuzwa kazi.
Baada ya kusimamishwa kazi kwa maofisa hao, Bodi ya Tanesco ilimpa kazi CAG kuchunguza tuhuma zilizokuwa zinawakabili pamoja na Mhando. Hata hivyo, Bodi ilisema kwa kosa alilolifanya Mhando hawezi kushtakiwa mahakamani kwa sababu makosa aliyoyafanya ya kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi ni kosa la kiuadilifu.
MWANANCHI

1 comment:
Hapo ndiyo mnapotuchanganya kwa kufikiri waTanzania wote ni mbumbumbu.. Mnatuambia mgongano wa kimasilahi ni kosa la kiuadilifu si kosa la jinai.. huu ni wizi wa mchana.. mkurugenzi ameiba tenda ..amejinufaisha mwenyewe , ameipa Kampuni inayomilikiwa na mke wake tenda za Kampuni ya umma wa waTanzania.. msifikiri sisi ni mambumbu wa sheria.. CAG anamaslahi hapa.. Takukuru nayo imelala.. uwizi wa mchana huu.
Post a Comment