ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 15, 2013

Mahabusu Keko wagoma kula

NA THOBIAS MWANAKATWE
Mahabusu 50 waliopo katika gereza la Keko, jijini Dar es Salaam wanaokabiliwa na kesi za mauaji na dawa za kulevya wamegoma kula wakishinikiza Jaji Mkuu, Othuman Chande, aingilie kati ili kesi zao zisikilizwe haraka.

Kati ya mahabusu hao waliogoma 22 ni raia wa Tanzania na 28 wanatoka katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini, Ireland,Nigeria, Kenya,Uganda, Liberia, Ghana, Iran, Pakstani, Indonesia na Guinea Bissau.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata kutoka katika gereza hilo na kuthibitishwa na baadhi ya askari magereza, mahabusu hao walianza mgomo huo rasmi jana ambao haijafahamika utakwisha lini.

Mkuu wa gereza la Keko, Ubwana Senshida, alipoulizwa, alisema suala hilo hawezi kulizungumzia kwa kuwa ndani ya Jeshi la Magereza msemaji ni mmoja tu ambaye ni Omary Mtiga.
“Mgomo huo hata kama upo, lakini sisi ndani ya Jeshi la Magereza tuna utaratibu kwamba msemaji wetu ni mmoja tu ambaye ni Mtiga ndiye anaruhusiwa kuzungumzia mambo yote ya jeshi, mtafute atakupa maelezo yote,” alisema Senshida.

Hata hivyo, Mtiga, alipotafutwa alisema suala la mgomo wa mahabusu hao atalitolea maelezo rasmi leo baada ya kuwasiliana na viongozi wa gereza la Keko.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alisema mara nyingi mahabusu wanapogoma hupeleka malalamiko yao kwa Jaji Kiongozi kwa ajili ya kushughulikiwa.

“Kama kweli mgomo wa mahabusu hao upo itakuwa malalamiko hayo yamepelekwa Jaji Kiongozi na mara nyingi wamekuwa wakifanya hivyo, nitawasiliana na uongozi wa gereza hilo kupata taarifa rasmi,” alisema.

Taarifa zaidi ambazo gazeti hili inazo ni kwamba mahabusu hao wamefikia hatua ya kugoma kutokana na kesi zao kuchukua zaidi ya miaka sita bila kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mahabusu hao walisema wamekuwa wakipata usumbufu kutokana na kutojua hatma ya kesi zao na kwamba mamlaka zinazohusika haziwapi maelezo ya kutosheleza sababu za kutosilizwa kwa kesi zao.. Kutokana na hali hiyo wamesema njia pekee ya kufikisha kilio chao kwa viongozi wa juu wa mamlaka za mahakama ni kugoma kula ili ziingilie kati.

No comments: