ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 6, 2013

Ni sahihi Wabunge wa Zanzibar kutunga Sheria za Tanzania Bara?


Wakati mjadala wa kuijadili Katiba ya Tanzania ukiendelea kwa uwazi kote nchini si vibaya tena tukalirejea suala la Muungano ambalo ni moja ya mambo yenye utata na yanayovuta hisia za wengi, Bara na Visiwani.
 
Ndiyo maana basi, matatizo ya Muungano yamejadiliwa na kutolewa  mapendekezo lukuki kama vile ndani ya Ripoti ya Jaji Nyalali iliyopendekeza  kuboresha Katiba yetu, Katiba ya Zanzibar ya 1984, Sheria ya Mapitio ya Katiba ya 2012 (Constitutional Review Act, 2012( na ile ya Shellukindo katika changomoto za muungano, ukiachilia utafiti wa wasomi kama Profesa Issa G. Shivji (angalia Tanzania: The Legal Foundations of the Union,tafsiri Kiswahili ikiwa ni 'Misingi ya Kisheria ya Muungano wa Tanzania (1990); Dk. Sengondo Mvungi, "Legal Problems of the Union Between Tanganyika and Zanzibar (  tafsiri-  "Matatizo ya Kisheria katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar"  ambayo tuliitafsiri kiasi hapa majuma machache yaliyopita). 
 
Na tena, muungano, dosari zake na fursa za maboresho umejadiliwa na Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo (machapisho mengi muhimu ya Katiba), hayati Profesa Haroub Othman (The Withering Away of the Union ('Kumomonyoka kwa Muungano'),  Wolfgang Dourado (the Consolidation of the Union, tafsiri Kiswahili ikiwa ni "Kushikamanishwa kwa Muungano") na Aboud Jumbe ('The Partnership: Tanganyika Zanzibar Union, 30 Turbulent Years ' , tafsiri yake Kiswahili ikiwa ni 'Ubia': Tanganyika na Zanzibar, Miaka 30 yenye mawimbi) na Martin Bailey (The Union of Tanganyika and Zanzibar: A Study in Political Integration', tafsiri Kiswahili ikiwa ni Muungano wa Tanganyika  na Zanzibar: Utafiti wa Kisomi katika Muungano wa Kisiasa" ). Dk, Mohammed Bakari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam naye ameliandikia sana jambo hili.
 
Gwiji mwingine wa Katiba Tanzania, Profesa Pala John Kabudi alitumia takribani miaka miwili kuutafiti na kuuandikia muundo wa Muungano wa Tanzania katika utafiti wake wa Shahada ya Pili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
 
Mwishoni mwa utafiti wake, aliona utata ulioko katika muundo huu na hivyo basi, kuamua kutoa ripoti inayouliza swali kwa kuwaachia wananchi wenyewe kuamua hatma ya aina ya Muungano wa Tanzania. Ripoti ya Utafiti wake ina jina la International Law Examination of the Union of Tanganyika and Zanzibar: A Federal or Unitary State? (1986). 
 
Ukiachana na hayo, tuibue sasa suala moja ambalo halijaonekana kama zito, lakini inastahili kupewa uzito na ufafanuzi wenye mantiki kwa raia. 
 
Suala hili si jingine, bali ni swali lililopo hapo juu: Je, ni vema, sahihi ama ni haki kwa raia wa Tanzania walioko Tanzania Bara (Tanganyika kabla ya Aprili 26, 1964)  kutungiwa Sheria na Wabunge wa visiwani waliomo ndani ya Bunge la Muungano  
wanaposhiriki katika kujadili, kupiga kura na kupitisha au kukwamisha muswada wa Sheria ambayo inatumika Tanzania Bara pekee na isiyotumika Zanzobar wala kugusa jambo lolote chin ya mambo ya Muungano kam yalivyoainshwa katika Jedwali la Kwanza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977? 
 
Kwa hakika, jibu la swali hili lapaswa kuwa hapana katika kudumisha haki sawa kwa raia wa pande zote mbili za muungano, uondoaji wa kero za Muungano na pia kuulinda ama kuuboresha muungano wenyewe ambao umetwajwa kuwa na dosari kadhaa wa kadhaa. Nilifafanue zaidi jambo hili hapo juu.
 
Mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano
 
Mkataba wa Muungano (Articles of the Union) uliosainiwa Aprili 22, 1964, siku nne tu kabla ya Muungano wenyewe kuzinduliwa rasmi, uliainisha mambo ya Muungano (yale yaliyostahiki kushirikisha pande zote mbili) na mambo yasiyo ya muungano (yale ambayo Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kila mmoja alikuwa huru kuyafanya kana kwamba ni nchi huru inayojitegemea na bila kuingiliwa ama kuhojiwa na upande mwingine). Mfumo huu ndio tulionao hadi sasa.
 
Utaona basi kuwa, orodha ya mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano yalikuwepo tangu 1964, yaani miaka 13 hivi kabla ya kuwepo kwa Katiba ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo ilikuja kuyaainsha kwa ufasaha zaidi mambo hayo (Angalia Jedwali la Kwanza la katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, toleo la mwaka 2005 linalotumika sasa).  
Ni muhimu kutaja tu hapa kuwa kabla ya Katiba ya sasa  pande zote mbili zilikuwa zikiongozwa na Katiba ya muda, yaani katiba ya mpito ya mwaka 1965 (Interim Constitution of 1965).
 
Kuwepo kwa orodha ya mambo ya muungano na yasiyo ya muungano (yaani mwaka 1964) kabla ya kutengezwa kwa katiba mahsusi  mwaka 1977) ambayo ingebainisha haki na wajibu katika utekelezaji wa mambo hayo pengine ni jambo lililochangia kwa kiasi fulani kuwepo kwa dosari zilizopo sasa. Kimtizamo binafsi, hii ni sawa na mtu kujenga nyumba iliyo kama ukumbi mkubwa wa dansi halafu akaja kuanza kuandaa mipango ya kuanza kupanga ugawaji wa vyumba, jiko na maliwato  baadaye kabisa wakati tayari nyumba hiyo imeshaezekwa na kuwekewa milango na madirisha. 
 
Hii ni dosari ambayo inashabihiana na ukosefu wa uhandisi wa awali katika mchakato  (front design engineering), utaalamu katika fani ya uhandisi ambao  usipofanyika hutafsiriwa kama kuandaa majanga kwa kila kitakachofuata baadaye.  Na ndiyo maana basi utaona kuwa watafiti wengi wameainisha mapungufu kama tulivyowaorodhesha hapo juu. 
Na ndiyo maana utaona pia kuwa mambo ya Muungano yamekuwa yakiongezwa kila baada ya muda fulani na yamekuwa mengi mno kiasi kuwa, Profesa mmoja maarufu kutoka Zanzibar alizungumza Dar es Salaam hivi karibuni kuwa, hili ni jambo linalowaumiza Wazanzibari wengi kwa vile kila jambo fulani linapofanywa ni la muungano, linamaanisha Rais na Serikali ya Zanzibar (SMZ) wanaondolewa mamlaka ya mwisho na kutafsiriwa kuwa  wamemezwa na Serikali ya Muungano. 
 
Kwa siku za karibuni mathalani suala la Utafiti wa Mafuta na gesi limekuwa tata, ikiwa ni miaka michache tu baada ya mgogoro wa 1993 Zanzibar ilipojiunga na Umoja wa Nchi za Kiislam Duniani (IOC) na kutajwa imekiuka makubaliano ya Mkataba wa Muungano kwa kushiriki kusaini mkataba wa Kimataifa jambo ambalo lilipaswa lifanywe na mamlaka za Muungano inayoundwa chini ya Ibara ya 34 ya Katiba ya Muungano,  Ibara ndogo ya 34 (1) inaeleza kuwa mamlaka yake yatakuwa juu ya mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Jedwali la Kwanza la Katiba ya Muungano ya mwaka 1977. 
 
Kwa muda sasa, mambo haya ya Muungano yamekuwa ni 22 na ni pamoja na Katiba yenyewe ya Muungano ya 1977, Uhusiano wa Nje/Kimataifa, Ulinzi na Usalama, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya kutangaza Hali ya hatari/dharura, uraia, uhamiaji, ukopaji fedha nje ya nchi na biashara za kimataifa, kodi za mapato, bandari, usafiri wa anga  na  posta na simu.
Nyingine ni  sarafu, fedha na sekta ya benki, ubadilishanaji wa fedha kati ya Tanzania na fedha za nje na udhibiti wake, leseni za viwanda na takwimu, elimu ya juu, raslimali za mafuta na gesi asilia, Baraza la Mitihani la Tanzania pamoja na kazi zote za Baraza hili; utafiti, hali ya hewa, takwimu, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania pamoja na Usajili wa Vyama vya siasa na masuala yahusianavyo na vyama hivi.
 
Tukirejea katika swali letu hapo juu, kwa masuala ya Tanzania Bara na Sheria zinazotumika huko, mamlaka na utnguaji wa sheri hizo unapaswa kufanywa na  Serikali ya Muungano inayotajwa kuwa na mamlaka ya mwisho juu ta Mambo ya Muungano na pia yote yasiyo ya muungano kuhusiana na Tanzania Bara (zamani Tanganyika).   
 
Ikumbukwe kuwa Tanzania kuna sheria za aina mbili na mamlaka pia vyombo viwili tofauti vya kutunga sheria hizo. Kwanza, kuna sheria zinazotumika Zanziobar pekee na zisizo za muunganio wala kuhusiana na watu au eneo la kijiografia la Tanzania Bara. 
 
Mfano wa heria hizo ni masuala ya afya na utabibu, elimu ya awali na ya kati, sheria za kifamilia, sheria ya jinai za Zanzibar (Penal Decree), masuala ya maji na pia ardhi ya Zanzibar. Sheria hizi hutungwa na Baraza la Wawakilishi (Bunge la zanzibar) liloundwa chini ya Ibara ya 106 ya Katiba ya Muungano wa Tanzania na madaraka yake kufafanuliwa katika ibara hiyohiyo pamoja na ile ya 107.  
 
Itakumbukwa kwa Wawakilishi hupigiwa kura na watu wa Tanzania visiwani pekee kwa taratibu tofauti na Sheria za uchaguzi zinazotumika Bara na pia hata siku tofauti ya uchaguzi mkuu. 
 
Katika hili, hakuna mbunge wa Tanzania bara anayeshiriki kutunga kwa vile sheria hizi ni za watu wa Tanzania visiwani pekee.
 
Kwa upande mwingine, Sheria zinazotumika Tanzania bara kwa masuala yasiyo ya Muungano na yasiyohusika Zanzibar. Sheria hizi ni pamoja na Sheria ya Jinai ya Tanganyika/Tanzania Bara maarufu kama Penal Code (Sura ya 16), na Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971. 
 
Sheria hizi ni mahususi kwa watu na eneo la kijiografia la Tanzania Bara tu. Ndiyo kusema mkazi wa Wete, Pemba au Unguja Mjini Magharibi, hawezi kushtakiwa chini ya sheria hizi akiwa Visiwani ingawa atashtakiwa akizivunja akiwa Tanzania Bara.
Walakini uliopo katika jambo hili ni kuwa hakuna Bunge mahsusi la Tanzania bara katika utungaji wa Sheria hii kama ilivyo kwa watu na himaya ya visiwani. 
 
Badala yake, sheria hizi za Bara pekee hutungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoundwa chini ya Ibara ya 62 ambalo ndani yake wamo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Zanzibar na ambao wamepigiwa kura na watu wa Zanziobar pekee, kwa taratibu na mazingira yaliyopo Tanzania visiwani pekee lakini wakiingia ndani ya Bunge la Muungano kupitia nyadhifa zao hizo za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. 
Si kosa kwa Wawakilishi-wabunge hawa kuwemo ndani ya Muungano kwa masuala, mijadala na utungaji wa Sheria za Muungano kwa sababu yote haya huathiri maslahi ya watu na eneo la kijiografia wanakotoka na pia kama wabia wa Muungano wenyewe.
 
Lakini je, ni halali kwa Mbunge wa Pemba au Unguja kutunga sheria itakayoathiri mgawanyo wa ardhi ya kimila inayotumika Kagera au Lindi? Au sheria itakayohusika kuamua kama mkazi fulani wa Kariakoo ya Tanzania Bara (si Kariakoo ya Zanzibar) kama aende jela Ukonga miaka 30 au la. 
 
Je, ni halali kwa Mwakilishi huyo kutunga sheria inayohusika na ndoa ya watu fulani waishio Tanga au Tabora wakati wawakilishi wa maeneo hayo hawahusiki kutunga sheria za Tanzania Visiwani?  
 
Jambo hili si la kudharau kulizungumza kwa sababu mamlaka ya utungaji sheria za nchi hutokana na ridhaa za yule anayetungiwa  na pia ukweli kuwa kwa vile katika nadharia ya usawa wa sheria mtunga sheria na mtungiwaji sheria huwajibishwa sawa, nadharia hii inakosa mantiki kwa sababu mtunga sheria wa visiwani hatajali kama sheria fulani anayoitunga ya jinai itamuumiza mtu wa bara kwa sababu yeye hahusiki nayo moja kwa moja kwa ukaribu.
 
Na ndiyo maana sasa, hata katika miungano mingine, mathalani Marekani, utaona mtunga Sheria anayechaguliwa na watu wa jimbo la Texas anahusika katika utungaji wa Sheria za Serikali ya Shirikisho ya Marekani (Federal Government) zinazotumika pia Hawaii, Florida na majimbo mengine yote ya Marekani lakini hata siku moja hawezi kukaa Austin, Texas (linapokaa bunge la jimbo hilo) na kuwatungia sheria watu wa California au New York kwa masuaala yasiyohusika ya serikali ya Shirikisho na ambayo hata Rais Obama mwenyewe anaweza asiwe na mamlaka nayo.
 
Nilikuwa nazungumzia hapa Wabunge watano wanaochaguliwa  na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake na ambao huingia ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 66(1)(c ) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
 
Denis Maringo ni Mwanasheria. Simu: 0765172591; 0719270067; barua-pepe: dnmaringo@gmail.com
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: