ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 6, 2013

TISA WAFA MAJI, KUZAMA KWA BOTI ZIWA TANGANYIKA


Watu tisa wamekufa maji baada ya boti ya MV Yarabi Tunusuru kuzama kwenye Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Fraisser Kashai, alitaja idadi ya vifo hivyo na kueleza kuwa miili ya watu hao imepatikana ambapo saba kati ya hiyo ni wanawake na miwili ni watoto wa kiume.
Aliiambia NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu kutoka Kigoma kuwa maiti nane za wanawake na ya mtoto mmoja wa kiume zimetambuliwa na jamaa zao.
Alisema miili hiyo ilipatikana juzi kwenye eneo la ajali kijijini Herembe wilayani Uvinza mkoani Kigoma na kwa sasa imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa huo ya Maweni.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni pamoja na Mwalimu Mzinga Kandoro, aliyeelezwa kuwa anafundisha katika Shule ya Msingi Filbert Bayi ya Dar es Salaam.
Wengine ni Mary Kawaya, Shami Baba maarufu kama Mama Baba wote wakazi wa Kirando wilayani Nkasi, pia yupo raia wa Burundi aliyejukana kama Wa Mjini, wengine ni Sarah Joseph na Mama Seba, wote wenyeji wa Karungu Nkasi mkoani Rukwa na mtoto Shadrack Amyashi.
Akizungumzia mkasa huo alisema:
TUKIO LA AJALI
Boti hiyo iliondoka katika kijiji cha Mwambao cha Kipiri Kirando kilichoko mkoani Rukwa Jumatano saa 10 jioni ikipitia mji wa Rumonge ulioko nchini Burundi na baadaye kuelekea mji wa Uvira ulioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa Kamanda, Alhamisi saa 4:00 usiku iliwasili kijiji cha Herembe kilichoko tarafa ya Buhingu Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma lakini ilizama baada ya kupigwa na dhoruba ikiwa na tani 45 za shehena na abiria 85.
Kashai alisema kati ya abiria hao, 64 wamenusurika, tisa walifariki na zaidi ya 10 hawajulikani waliopo na kuongeza kuwa Ziwa Tanganyika lina upepo mkali na mawimbi makubwa ambayo yaliyumbisha boti hiyo na kuizamisha.
UOKOAJI
Kamanda alisema kijijini Herembe hakuna mawasiliano kutokana na kukatika madaraja na kuharibika kwa barabara kulikosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, hali inayokwamisha kuwahi kwenye tukio kwa ajili ya uokozi.
Aliongeza kuwa uokoaji wa kutafuta abiria unafanywa kwa ushirikiano baina ya askari wa JWTZ wa Kikosi cha Kigoma, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini na Nchikavu (Sumatra).
MMILIKI
Kamanda wa Mkoa wa Kigoma alimtaja mmiliki wa boti hiyo kwa jina Msiwa Khamisi mkazi wa Ujiji Kigoma na kuongeza kuwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano na uchunguzi .
Halikadhalika nahodha wa chombo hicho Seif Akilimali (34) ni miongoni mwa walionusurika na pia anasaidia kwenye uchunguzi unaofanywa baina ya polisi na Sumatra.
MAELEZO YA Sumatra
Meneja Uhusiano wa Sumatra, David Mziray, alisema boti iliyozama ilijulikana kwa jina la Yarabi Tunusuru na ilikuwa inamilikiwa na Msiwa Khamisi mkazi wa Ujiji Kigoma.
Alisema boti hiyo ilisajiliwa Oktoba mwaka jana kwa utambulisho namba KST 0029 na ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 50.
Mziray alisema jana saa 5:00 asubuhi kituo cha Sumatra cha ufuatiliaji na uokozi cha Dar es Salaam kilipokea taarifa ya kutokea ajali ya boti hiyo kutoka kwa Ofisa wake wa Kigoma Adam Mwamilo.
Alisema katika ajali hiyo abiria 66 waliokolewa wakiwa hai na kwamba saba hawajulikani walipo na tisa walipoteza maisha.
Chanzo cha ajali kwa mujibu wa mamlaka hiyo hakijafahamika na uchunguzi kuhusu ajali hiyo unaendelea.
ENEO LA AJALI
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Herembe na kwamba boti ilikuwa ikitokea Kalungu mkoani Katavi kuelekea Rumonge nchini Burundi.
Maelezo ya mamlaka hiyo yanatofautiana na ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma yanayoeleza kuwa boti ilikuwa na abiria 85 wakati Sumatra ilisema walikuwamo 82.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: