ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 3, 2013

Salamu za mwaka mpya wa 2013


"Rais
Nimefarijika kwa hatua kubwa za maendeleo ambazo nchi yetu imefikia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaomalizika katika sekta mbali mbali za maendeleo, kiuchumi, kijamii na katika uimarishaji wa miundo mbinu na huduma za jamii.  Nitayaeleza baadhi ya mafanikio hayo   katika sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi yetu matukufu hapo tarehe 12 Januari, 2013.  Kwa kifupi tu, tumekuwa na mafanikio ya kuridhisha katika kuimarika kwa huduma za jamii zikiwemo huduma za afya, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama, nakadhalika. Vile vile, chakula cha kutosha kinapatikana kutokana na juhudi za wakulima wetu na jitihada za wafanyabiashara. Ustawi wa uchumi wetu na biashara ya karafuu na utalii pia unaridhisha.

SALAMU ZA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN
KATIKA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2013
 
 
Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu (SW). Mwingi wa  rehema na utukufu kwa kuendelea kuturuzuku neema ya uhai hadi muda huu ambapo tunauaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2013. Neema hiyo ni kubwa kwani hivi karibuni pia tuliukaribisha mwaka mpya wa 1434 Hijiria. Mwaka huu wa Kiislamu ni adhimu kwetu na hapa Zanzibar ulipokewa na kusheherekewa kwa shamrashamra mbali mbali.   
 
Bila ya shaka hizi ni neema kubwa na fadhila Yake kwetu ambapo tunapaswa kushukuru kwani walikuwepo wenzetu wengi tulioanza nao mwaka huu na hivi sasa wameshatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mola wetu awape malazi mema walipo, awasamehe makosa yao pamoja nasi, na  atupe sote hatima njema duniani na akhera.  Tunamuomba awape wazee na wagonjwa wetu majumbani na hospitalini shufaa ya maradhi yao ili nao waendelee kufanya shughuli zao za kimaisha  pamoja nasi.
 
Ndugu Wananchi,
Kuingia katika mwaka mpya tukiwa na hali ya amani, umoja na mshikamano ni jambo linalonipa faraja kubwa. Napenda nitoe shukrani zangu za dhati na nikupongezeni ndugu wananchi kwa kuutambua umuhimu wa jambo hili kwa ustawi wa maendeleo yetu, usalama wetu na mali zetu na pia wa wageni wetu wanaofika nchini kwa shughuli mbalimbali na hasa utalii. Kadhalika, pia napenda niwashukuru viongozi wa dini mbalimbali kwa kuendelea kuwasihi waumini wao juu ya umuhimu wa amani na kuiombea nchi yetu salama.
 
 
Ndugu Wananchi,
Nimefarijika kwa hatua kubwa za maendeleo ambazo nchi yetu imefikia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaomalizika katika sekta mbali mbali za maendeleo, kiuchumi, kijamii na katika uimarishaji wa miundo mbinu na huduma za jamii.  Nitayaeleza baadhi ya mafanikio hayo   katika sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi yetu matukufu hapo tarehe 12 Januari, 2013.  Kwa kifupi tu, tumekuwa na mafanikio ya kuridhisha katika
kuimarika kwa huduma za jamii zikiwemo huduma za afya, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama, nakadhalika. Vile vile, chakula cha kutosha kinapatikana kutokana na juhudi za wakulima wetu na jitihada za wafanyabiashara. Ustawi wa uchumi wetu na biashara ya karafuu na utalii pia unaridhisha.
 
Napenda nikuhakikishieni kuwa neema, baraka na mafanikio zaidi yatapatikana nchini iwapo tutaendelea kushikamana na kusimamia amani na utulivu huku tukizidi kujituma katika shughuli zetu mbalimbali halali za kujitafutia maisha. Tayari tunaona neema ya kuwepo vyakula mbali mbali, kuimarika kwa biashara na shughuli nyengine za kijamii mambo ambayo jamii nyengine wanayakosa katika kipindi cha kumalizia mwaka.
 
Vile vile, nawakumbusha  wazazi wenzangu kufanya matayarisho ya skuli kwa watoto wetu. Najua wanafunzi wapya wameshaandikishwa na walioko skuli wanaingia kwenye madarasa mapya. Wote hawa wanahitaji wapate vifaa mbali mbali vinavyohitajika. Aidha, wanafunzi wote waliofanya mitihani yao tunawaombea mafanikio na wanaoendelea na masomo waongeze bidii na kila wakati wakumbuke kuwa bidii ndiyo siri ya mafanikio.
 
 
 
Ndugu Wananchi,
Ukuaji wa maendeleo katika nchi yoyote hutegemea  sana kuimarika kwa hali ya amani na utulivu  katika nchi. Pamoja na kufanywa kwa vitendo vilivyolenga kuvunja amani na utulivu nchini katika  nyakati mbali mbali kwenye mwaka tunaoumaliza, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeidhibiti hali hio na inaendelea vizuri.  Nchi yetu inaendelea kuwa na hali ya amani  na utulivu.
 
Kwa mara nyengine napenda kutoa pole kwa wananchi wote walioathirika kwa namna mbali mbali kutokana na vitendo vya ghasia na uvunjaji wa amani vilivyosababisha hasara kubwa na usumbufu kwa wananchi.  Navipongeza vikosi vyetu vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri walioifanya katika  kuirudisha  hali ya amani na utulivu nchini.
 
Nakusihini wananchi nyote muendelee kushirikiana na Serikali katika kuzuwia vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria kwa kuelewa kuwa huo ni wajibu wa raia wema na kufanya hivyo kutachangia kuwepo kwa hali ya amani , utulivu na mshikamano ambavyo ndivyo siri kubwa na mafanikio tuliyokwisha kuyapata.
 
Ndugu  Wananchi,
Nchi yetu imeendelea kujijengea taswira njema kwa marafiki zetu na taasisi mbali mbali za Kimataifa kutokana na mafanikio tuliyoyapata baada ya kuanzishwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa. Serikali ambayo  imekwishatimiza miaka miwili na tayari tumeanza mwaka wa tatu.
 
 
Nimekuwa nikisema mara kadhaa kuwa tunapokea wageni, mialiko na pongezi kutoka nchi mbali mbali ambao wamekuwa wakionesha kuridhika na hali ya mafanikio yetu. Ni vyema mafanikio haya tukazidi kuyaendeleza kwa faida ya kila mmoja wetu. Lazima tuoneshe kuzidi kuaminiana na kuongeza umoja na ushirikiano wetu kwa kadri tunavyokwenda mbele. Kwa pamoja tuwe  na dhamira ya dhati ya kutopenda kurudi nyuma tulikotoka na nia yetu sote iwe ni kwenda mbele zaidi.
 
Ndugu Wananchi,
Katika kuukalimilisha mwaka huu wa 2012, natoa shukrani kwa viongozi wa ngazi mbali mbali wa    serikali, watendaji katika ngazi zote za Serikali, viongozi wa Serikali za mitaa na taasisi mbali mbali za kijamii na washirika wetu wa maendeleo kwa ushirikiano na mchango wao muhimu waliotoa katika kufanikisha utekelezaji wa mipango na shughuli mbali mbali za Serikali katika kipindi cha mwaka mzima.
 
Kwa mara nyengine, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu ndugu wananchi kwa kushirikiana na  Serikali yenu.  Jambo hilo limetusaidia sana na linatupa moyo na ari zaidi ya kukuhudumikieni kwa kuelewa kuwa hilo ni jukumu letu muhimu  tunalopaswa kukutekelezeeni kwa mujibu wa Katiba na ahadi tulizotoa kwenu.
 
Napenda kukuahidini kuwa jukumu hili tutaendelea kulitekeleza kwa bidii na uwezo wetu  wote hivi sasa  na mwaka ujao, tukiamini kuwa tuna dhamana ya kuendelea kutekeleza wajibu wetu kwa maslahi ya nchi yetu.
 
Ndugu Wananchi,
Nakusihini sana muendelee kushirikiana na Serikali yenu katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuzitumia fursa zilizopo za kujiletea maendeleo yenu.  Napenda nikukumbusheni wajibu  wenu wa kuilinda miundo mbinu mbali mbali iliyojengwa kwa gharama kubwa zikiwemo barabara, nguzo za umeme, waya, na kadhalika vilivyojengwa katika sehemu unamopitia mtandao wa Serikali(e- Government) na umeme kwenye maeneo mbali mbali nchini.  Kadhalika, sote tuwe walinzi wa rasilimali zetu na tuhimizane kuzingatia taratibu za kisheria katika matumizi bora ya rasilimali hizo kwa faida yetu na vizazi vijavyo.
 
Napenda kukamilisha salamu zangu kwa kukutakieni nyote kheri ya mwaka mpya wenye mafanikio, kheri na baraka zaidi. Namsihi kila mmoja wetu atie nia ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zake popote alipo. Kadhalika, napenda kukutanabahisheni kuwa katika kusherehekea mwaka mpya mzingatie maadili yetu na taratibu za kisheria ziliopo.  Jeshi letu la Polisi litaimairisha doria na kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjaji wa sheria na vinavyohatarisha amani na utulivu nchini vinadhibitiwa. Nawasihi watu wote washerehekee mwaka mpya kwa amani, mapenzi baina yetu na umoja na haya yawe malengo yetu makuu kwa ajili ya maendeleo yetu.
 
                   “HERI     YA      MWAKA     MPYA”
                                 Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments: