ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 31, 2013

Uuzaji wasichana: Wenyeviti kikaangoni

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema

Serikali wilayani Temeke jijini Dar es Salaam imesema itafanya uchunguzi ili kuwabaini baadhi ya wenyeviti wa serikali za mitaa wilayani humo wanashirikiana na mawakala wanaosafirisha watoto kwenda nje ya nchi kutumikishwa.

Wenyeviti hao wanatuhumiwa kughushi barua na kuwapatia mawakala hao zikionyesha kuwa wanasafiri kihalali kwenda Zanzibar kabla ya kupelekwa Uarabuni kwa ajili ya kutumikishwa.


Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia Mjema, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na NIPASHE iliyotaka kujua hatua zinazokwisha kuchukuliwa na serikali juu ya baadhi ya wenyeviti wa serikali wilayani humo wanaodaiwa kutoa barua kwa watoto wanaonunuliwa na mawakala kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi za Uarabuni.

Mjema alisema kuwa hawezi kukataa kama wapo baadhi ya wenyeviti wanaofanya hivyo, lakini ili kupata ukweli wa jambo hilo serikali italifanyia uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

Katika uchunguzi ambao umeendelea kufanywa na NIPASHE kuhusu biashara ya binadamu, imebainika kuwa watoto wanaonunuliwa na mawakala kutoka mikoani wakifikishwa Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Zanzibar mawakala wanawatafutia barua kutoka kwa wenyeviti hao ili wasisumbuliwe bandarini kwahawana vitambulisho.

Uchunguzi huo umebaini kuwa biashara hiyo iliibuka kuanzia Desemba mwaka jana na kushika kasi Januari mwaka huu na wanaosafirishwa wengi ni watoto wa kike kutoka mikoa mbalimbali nchini. Wapo wachache wa kiume pia.  Uchunguzi huo ulibaini kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa na mawakala kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchi za Uarabuni kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za ndani ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora, Ruvuma, Tanga na Shinyanga.

Taarifa zinaonyesha kuwa mawakala hao wakishafanikiwa kuwapata watoto hao kutoka katika mikoa hiyo huwapeleka jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwa usafiri wa majini kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Watoto hao wakifikishwa Zanzibar hukutana na watu maalum ambao huwapokea na kufawanyia mipango ya kuwasafirisha kwa usafiri wa ndege au wa majini kwenda Uarabuni ambako hutumikishwa kazi mbalimbali.

Mawakala hao wakishafanikiwa kuwasafirisha kutoka Bandari ya Dar es Salaam hulipwa wastani wa Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 8) kwa kila mtoto wanayefanikisha kumvusha kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita wastani wa watoto kati ya watano hadi 10 hufika katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kila siku.

NIPASHE ina taarifa za kina za watoto wenye umri kati ya miaka minane na 15 kutoka kijiji cha Nakapanya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma;  mkoa wa Tabora; kutoka kijiji cha Mkangula Mkoa wa Mtwara na kijiji cha Mbembaleo pia cha mkoani Mtwara.

Pia wamo kutoka kijiji cha Manoro Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga; kutoka Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma; kutoka kijiji cha Namalumbusi Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara na kutoka Mkoa wa Manyara.

Wengine waliokwisha kukamatwa wanatoka kijiji cha Ndanda Mkoa wa Mtwara; kijiji cha Mteruka wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi na kutoka kijiji cha Mnazi mmoja Mkoa wa Mtwara.

Wapo pia kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Mtwara, kutoka kijiji cha Kokoro wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga na mwingine mkazi wa Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.

Juzi Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Maji, Mboje Kanga, aliliambia NIPASHE kuwa mawakala watano wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo. Alisema kuwa mawakala waliokamatwa ni wakazi wa Zanzibar na kwamba hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi yao.

Kamanda Kanga ambaye hata hivyo, hakutaja majina ya mawakala hao, alisema kuwa walikamatwa kati ya Januari 23 na 24, mwaka huu wakiwa na watoto watano ambao waliwanunua kutoka mikoani.  Alisema watoto ambao ni wanafunzi wa shule za msingi, walikamatwa wakitaka kusafirishwa na mawakala hao kwenda Zanzibar, umri wao ni kati ya miaka 14 na 15 na walitoka katika wilaya za mikoa ya Ruvuma, Tabora na Mtwara.

Aliongeza kuwa katika mahojiano na watoto hao walisema kuwa walipata ridhaa ya kuchukuliwa na mawakala hao ambao haijafahamika baada ya kusafirishwa kwenda Zanzibar wangepelekwa katika nchi gani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: