ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 30, 2013

VALENTINE’S DAY HIYOOO! VIPI KUHUSU UHURU WA SIMU YAKO?

ZIMEBAKI siku kadhaa kabla ya kuadhimisha Siku ya Wapendanao Duniani (Valentine’s Day). Siku hii maalum ya ‘ku-show love’ huadhimishwa kila ifikapo Februari 14 ya kila mwaka ikiwa ni mahsusi kabisa kuonesha namna unavyompenda mpenzi wako au watu wengine muhimu maishani mwako.
Tunapojiandaa kuelekea siku hiyo, si vibaya tukakumbushana mambo ya msingi ambayo yatakufanya wewe na umpendaye muiadhimishe kwa uhuru. Katika siku za hivi karibuni, marafiki wengi wamekuwa wakinitumia ujumbe mfupi wa maneno na kunilalamikia jinsi wapenzi wao wanavyowanyanyasa kupitia simu zao.
Dada Irene wa Sinza, Dar aliniandikia kuwa mpenzi wake amekuwa na kawaida ya kuweka password kwenye simu yake kiasi kwamba hata akitaka kuigusa simu ya mpenzi wake, hawezi kufanya hivyo kwani hukataa kabisa kumtajia namba ya siri.
Akazidi kufunguka kuwa kibaya zaidi, mpenzi wake anapopigiwa simu wakiwa pamoja, hutoka na kwenda kuzungumza bafuni au nje kabisa huku akitumia sauti ya kunong’ona. Akaomba ushauri juu ya tafsiri ya tabia hiyo ya mpenzi wake.
Kaka Bariki kutoka Sumbawanga yeye alinitumia ujumbe na kunieleza kuwa mpenzi wake huwa anafuta meseji kwenye simu yake kila zinapoingia au anapotuma, wakati mwingine hubakiza zile alizomtumia yeye tu. Kama hiyo haitoshi, pia hufuta hata rekodi za simu zilizoingia au kutoka kwenye simu ya mpenzi wake.
Marafiki, hao ni baadhi tu ya wengi walionitumia ujumbe lakini wanawakilisha jamii yetu tunayoishi. Ni ukweli usiopingika kuwa matumizi ya simu yamerahisisha sana usaliti kwa wapenzi wasiojitambua. Simu zimefanya iwe rahisi mtu kutoka nje ya uhusiano wake na kulisaliti penzi lake.
Watoto wa mjini siku hizi wanakwambia ukishapata namba ya simu ya mwanaume au mwanamke ‘unayemtaka’, basi kila kitu kimeisha. Mipango yote hufanyika kwa SMS au wakati mwingine kupigiana, appointment hupangwa na mwisho wawili hukutana na kuvunja amri ya sita.
Walioachana kwa sababu ya simu ni wengi lakini pia wale ambao wanatifuana kila kukicha, kila mmoja akimfikiria mwenzake tofauti kuhusiana na matumizi mabaya ya simu idadi ni kubwa kuliko maelezo.
Leo nataka kuzungumzia kitu ambacho naweza kutofautiana na wengi lakini ndiyo ukweli hasa katika kipindi hiki, lengo ni kuleta amani na kuwafanya wapenzi na wanandoa kudumu kwa muda mrefu bila migogoro. Ninachotaka kusema ni kwamba mnapokuwa katika uhusiano kisha mkafikia hatua ya kufikiriana ndivyo sivyo kwa sababu tu ya simu zenu za mkononi ni hatari sana.
Kwa nini mpenzi wako afikie hatua ya kufikiria kwamba unamsaliti? Inawezekana ni kwa sababu ya namna unavyompa uhuru wa kuishika simu yako na kufanya anachokitaka. Kwa nini uweke password ambayo mpenzi wako haijui? Kwa nini ukazungumze na simu nje? Kuna kipi ambacho hutaki mpenzi wako akifahamu? Hizo ni tabia zilizopitwa na wakati.
Wapo wapenzi wachache ambao ni mfano mzuri wa kuigwa, yaani unakuta mtu anamuachia mpenzi wake simu hata kutwa nzima na anakuwa huru kabisa! Anafanya hivi kwa sababu anajiamini kuwa hana nyendo chafu na hamsaliti mpenzi wake. Itapendeza kila mmoja akiwa muaminifu kwa mpenzi wake hasa katika zama hizi zilizojaa maradhi sugu ikiwemo Ukimwi.
Ukimpa mpenzi wako uhuru kwenye simu yako, bila shaka hamtakwaruzana na mtasherehekea Valentine’s Day kwa mahaba ya dhati.

www.globalpublishers.info

No comments: