Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria wa treni hiyo walisema walifika Dodoma saa 9:00 usiku kuamkia jana wakitokea Bara kuelekea jijini Dar es Salaam.
Mariam Hassan, mmoja wa abiria kutoka Kigoma, alisema walijulishwa na uongozi wa TRL kuwa mataluma ya reli yamezolewa na maji ya mvua hivyo hakuna uwezekano wa kuendelea na safari hadi hapo eneo hilo litakapofanyiwa matengenezo.
“Kibaya zaidi kinachotusikitisha ni kuwa eneo hilo limekuwa ni kero kwa usafiri wa gari moshi kwa muda mrefu lakini serikali hailishughulikii ipasavyo na kusababisha wananchi kupata shida kama hii,” alisema.
Alisema baadhi yao wameishiwa fedha za chakula kwa kuwa walitegemea kuwasili jijini Dar es Salaam jana kulingana na ratiba ya treni hiyo.
Aliongeza kuwa hali hiyo imewafanya abiria hao sasa kugeuka ombaomba. Abiria mwingine, Maduka Mwanang’ayo, kutoka Mpanda, alisema kukwama kwa gari moshi katika kituo hicho cha Dodoma kumewasababishia kero nyingi.
Alizitaja kero hizo kuwa ni huduma za choo ni za kulipia katika kituo hicho pamoja na bei ya vyakula kupanda holela.
“Tangu tumefika hapa usiku tulitangaziwa kuwa haturuhusiwi kujisaidia kwenye vyoo vilivyopo ndani ya gari moshi hivyo huduma hizo zinapatikana kwa kulipia katika vyoo vilivyopo katika kituo hicho na abiria takayekutwa akijisaidia pembeni mwa gari moshi, atatozwa faini ya Shilingi elfu thelathini,” alisema.
Naye Stesheni Masta wa Stesheni ya Dodoma, Flavian Nyawale, akizungumza na waandishi wa habari, alisema kukwama kwa gari moshi hilo kumetokana na mataluma ya reli kuzolewa na maji juzi katika vituo vya Godegode na Kidete.
Nyawale alisema gari moshi lililokwama kituoni hapo lilikuwa likitoka Mwanza, Kigoma na Mpanda.
Alisema baada ya gari moshi hilo kufika Stesheni ya Dodoma, walipata taarifa kuwa mataluma ya reli yamezolewa na maji ya mvua eneo la Godegode na kwa msingi huo isingewezekana kuruhusu liendelee na safari. Alisema mafundi wa shirika hilo wanaendelea kulifanyia matengenezo eneo hilo na wanatarajia yatakamilika mapema na walitarajia kuliruhusu garimoshi hilo kuendelea na safari zake jana 2:00 usiku.
Kuhusu kero wanazozipata abiria waliokwama katika stesheni hiyo, alisema shirika hilo limewapa Sh. 4,000 za chakula kila abiria.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment