ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 16, 2013

Dk. Mwakyembe 'hakuna kulala' awacharukia Uhamiaji


NA THOBIAS MWANAKATWE
Waziri wa Uchukuzi, Dk, Harrison Mwakyembe, amewaagiza wafanyakazi wanaotoa huduma katika mpaka wa Tanzania na Zambia ofisi za Tunduma kufanya kazi masaa 24.

Aliwaagiza kufanyakazi kwa muda huo ili kukabiliana na msongamano mkubwa wa malori unatokana na madereva kusubiri kukamilika taratibu za forodha kwa muda mrefu .

Alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea mpaka huo uliopo wilayani Momba mkoani Mbeya kuangalia sababu za kuwepo msangamano wa magari hayo yakwenda nje ya nchi pamoja na kutafuta ufumbuzi wa kero hiyo.Dk.Mwakyembe alisema njia ya kwanza ya kutatua tatizo hilo ni wafanyakazi wa idara za serikali zinazohusika na utoaji wa huduma mpakani hapo kufanya kazi saa 24 na utekelezaji huo ufanyike haraka.

Alieleza kufurahishwa na viongozi wa serikali za Tanzania na Zambia kupitisha azimio hilo na kutaka utekelezaji wake uanze haraka ili tuondoa msingamano wa malori .

Dk.Mwakyembe alisema katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayoukabili mpaka wa Tunduma, Jumatano ijayo atakuwa na mkutano na Waziri wa Wizara za Uchukuzi, Biashara na Fedha wa Zambia kujadili changamoto mbalimbali zinazoukabili mpaka huo na hatua za kuchukuliwa .

Alisema mambo mengine yatakayozingatiwa na serikali za Tanzania na Zambia katika kukabiliana na tatizo hilo ni kuifufua Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili shehena ambayo kwa sasa inasafirishwa na magari ianze kupelekwa kwa reli.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abihudi Saideya,alisema tatizo la msongamano wa malori katika mji wa Tunduma unatokea upande wa Zambia ambako kuna sehemu kwa ajili ya kuegesha maroli hivyo hata kama dereva amemaliza taratibu za uhamiaji upande wa Tanzania magari hayawezi kwenda Zambia kuegesha wakati wanasubiri taratibu za forodha.

Madereva walisema kutokana na kukaa muda mrefu mpakani posho za matumizi wanazolipwa na waajiri wao zinaisha wakiwa mpakani Tunduma.

No comments: