Stori: Timothy Itembe, Tarime
TAIFA linapita kwenye kipindi kigumu mno, raia wamekuwa wakilitunishia misuli jeshi la polisi, wakati ya Mtwara na Morogoro yakiwa hayajasahaulika, Tarime limezuka jambo lingine.Wakazi wa Tarime wakiwa na silaha zao za jadi wakati wakimsikiliza RPC na DC.
Mamia ya wakazi wa Tarime, Mara, wakiwa na silaha za jadi, walivamia Mbuga ya Wanyama ya Serengeti, wakikusudia kupambana na askari wa wanyamapori.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita ambapo kama si juhudi za jeshi la polisi kuwasihi wananchi hao wenye hasira, hali ingekuwa mbaya zaidi.
Jeshi la polisi Wilaya ya Tarime, lilipata taarifa wakati wananchi hao wakijiandaa kuingia ndani ya hifadhi, hivyo kuingilia kati na kutaka mazungumzo yafanyike.
Wananchi wa Tarime walitulia baada ya kuridhishwa na maelezo ya uongozi wa wilaya pamoja na jeshi la polisi kuwa uchunguzi utafanyika na watuhumiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mwili wa marehemu Matinde Mwita Marwa aliyeuawa kwa kupigwa risasi kichwani na askari wa wanayamapori.
CHANZO CHA MGOGORO
Wananchi hao, walikasirishwa na kitendo cha askari wa wanyamapori, kumpiga risasi kichwani mkazi wa Tarime, Matinde Mwita Marwa, 38, na kumsababishia kifo.
Marwa, alipigwa risasi baada ya kutokea mvutano kati ya askari wa wanyamapori na wananchi ambao walikuwa wanalisha mifugo katika eneo linalodaiwa kuwa ni la Mbuga ya Serengeti.
Kaka wa marehemu, Twani Mwita Marwa alisema mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Elyasi Goroyi, anayekaimu ukuu wa Wilaya ya Tarime kwamba ndugu yake alikuwa anachunga mifugo akiwa na wenzake.
Aliongeza kuwa walikuwa wanachunga ng’ombe karibu na mbuga hiyo, kwa hiyo askari wa wanyamapori waliwachukua wale ng’ombe na kuwaingiza kambini.
“Waliwaingiza kambini ili tukienda kuwakomboa, watutoze faini ya shilingi 30,000 kwa kila ng’ombe. Kutokana na hali hiyo, marehemu na wenzake walijaribu kujitetea ndipo ukatokea mvutano mkubwa.
“Wale askari walizidi kuwaswaga ng’ombe kuelekea kambini, marehemu na wenzake wakawa wanawazuia ndipo askari mmoja akampiga risasi marehemu, ikampata kichwani na kumsababishia kifo,” alisema Twani.
MKUU WA WILAYA ANENA
Kutokana na maelezo hayo, Goroyi alisema: “Naomba maafisa wa mbuga ya wanyama Serengeti mniletee ofisini kwangu ramani ambayo inaonesha mipaka ya mbuga pamoja na tangazo la serikali ambalo lilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali kubainishia mipaka ya hifadhi na makazi ya raia.”
KAMANDA ANENA
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha (pichani) aliwaambia wananchi kuwa atahakikisha upelelezi unafanyika kubaini chanzo cha tukio hilo na tayari linawashikilia watu wawili.
“Upelelezi ukikamilika wahusika watapelekwa mahakamani,” alisema Kamugisha.
Chanzo: Globalpublishers
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake