Mbunge wa Ziwani (Cuf), Ahmed Juma Ngwali
Mtandao wa Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini umewasiliana na wenzao wa Canada kushughulikia tuhuma zilizotolewa dhidi ya Mbunge wa Ziwani (Cuf), Ahmed Juma Ngwali, za kutorosha watoto wawili nchini humo.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa Interpol nchini zinaeleza kuwa katika mawasiliano hayo, mtandao huo umetuma kwa wenzao wa Canada vielelezo mbalimbali vinavyowahusu watoto hao, zikiwamo pasi zao za kusafiria.
Kwa mujibu wa habari hizo, vielelezo hivyo vilitumwa nchini humo Januari 30, mwaka huu.
Hata hivyo, habari zinaeleza kuwa hadi kufikia jana, Interpol nchini walikuwa bado hawajajibiwa na wenzao wa Canada.
Mkuu wa Interpol nchini, Gustavus Babile, alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana, alimtaka mwandishi kumuandikia barua ya kiofisi Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kama anahitaji kupata taarifa hiyo kutoka kwake (Babile).
NIPASHE iliwasiliana na Kaimu DCI, Isaya Mngulu, kwa njia ya simu jana, lakini alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kujibu swali lolote kwa kuwa anahudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka wa maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma.
Hata hivyo, Mngulu alimwelekeza mwandishi kuwasiliana na mmoja wa makamishna wa polisi waliokuwapo jijini Dar es Salaam jana.
Kamishna huyo wa polisi alipotafutwa, simu zake zote za kiganjani zilikuwa zikiita bila kupokewa.
Ngwali amefunguliwa jalada katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam, akituhumiwa kuvunja ndoa ya mfanyabiashara, Khalfan Said Chondoma wa mjini Unguja na kutorosha watoto hao nchini kwenda Canada, kinyume cha sheria.
Mbunge huyo anatuhumiwa na Khalfan, ambaye ni mkazi wa Saateni, kisiwani Unguja, kuingilia ndoa yake na kusababisha kuvunjika na hivyo kupata mwanya wa ‘kumpora’ mkewe.
Watoto anaotuhumiwa kuwatorosha ni msichana (8) na mvulana (9) baada ya kuwabadili ubini halali wa baba yao mzazi na kuwapachika ubini wake (Ngwali).
Khalfan (31) aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi Oysterbay na kufungua jalada namba OB/RB/21545/2012.
Alidai kabla ya matukio hayo, Ngwali alikuwa rafiki yake aliyekuwa akimtembelea nyumbani, lakini hakujua kuwa alikuwa ana lake moyoni dhidi ya mkewe.
Khalfan alidai wiki chache baada ya kuzuka mtafaruku kati yake na mkewe na kwenda nyumbani kwa wazazi wake, mkoani Tanga, alisikia kuwa ameolewa na Ngwali bila kumpa talaka.
Alidai watoto wake walitoroshwa kwenda Canada, Oktoba 30, mwaka jana na kwamba, hadi sasa bado wanaishi huko, ambako wao na mama yao wanajitambulisha kama wakimbizi.
Alidai kufuatia kitendo hicho, aliwasiliana na Interpol nchini, ambao aliwakabidhi vielelezo vyote vinavyohusiana na shauri hilo.
Khalfan alionyesha vielelezo mbalimbali, kikiwamo cheti cha ndoa kuthibitisha kuwa alifunga ndoa na Aisha Machi 11, 2004; pia vyeti vya watoto hao vya kuzaliwa kuthibitisha kuwa ni watoto aliowazaa na mwanamke huyo.
Kwa upande wake, Ngwali alithibitisha watoto hao pamoja na mama yao mzazi, Aisha kuwapo Canada.
Alidai Aisha ni mkewe halali wa ndoa, lakini watoto hao ni wa Khalfan.
Alidai hakumbuki tarehe na mwezi aliofunga ndoa na Aisha, lakini anachokumbuka ndoa yao ilifungwa miaka miwili iliyopita baada ya mwanamke huyo kumkataa Khalfan kutokana na kumzuia kufanya kazi ya duka.
Ngwali alidai ndoa kati yake na Aisha ilifungwa wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, kwa idhini ya wazazi wa mwanamke huyo.
Alidai cheti cha ndoa kinachothibitisha kuwa alifunga ndoa na Aisha kipo, lakini kwa kuwa yeye husafiri mara kwa mara, hawezi kutembea nacho mkononi.
Hata hivyo, alidai kuwa hakuishi muda mrefu na Aisha, kwani mwaka jana mwanamke huyo alifanya hadaa na kuondoka kwenye himaya yake na kwenda kuishi na watoto hao Canada, kinyume cha taratibu.
Alidai kufuatia kitendo hicho, aliuandikia barua Ubalozi wa Canada, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Jeshi la Polisi kuwaelezea kilichotokea kuhusiana na mwanamke huyo.
Anadai kuwa anacholilia Khalfan ni wivu tu wa mapenzi.
Alidai pia anamshangaa Khalfan kumtuhumu kwamba, amebadili majina ya watoto wake bila kuthibitisha tuhuma hizo.
Ngwali alidai ni jambo lisilowezekana kubadili majina ya watoto kwani ilitakiwa aende kufanya hivyo mahakamani na kusisitiza kuwa kama hilo litathibitika, atakuwa tayari kuwajibika.
Anadai kuwa anayosema Khalfan ni uwongo kwa kuwa anataka aonewe huruma na kwamba ni wivu tu wa mapenzi ndiyo unaomsumbua ingawa wote wamemkosa mwanamke huyo.
Ngwali alidai sehemu kubwa ya maelezo hayo aliyatoa alipohojiwa na vyombo vya dola, ikiwamo Interpol
1 comment:
Halfani acha uongo ulimkataa mwenyewe mwanamke ulipomuacha alikaa sana ndio akaolewa tena ulimpa talaka mpk watu wa kwao acha kuvuta bangi wewe
Post a Comment