Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuandaa mtaala maalum wa kuzuia vurugu nchini ambayo itafundishwa katika vyuo vya jeshi hilo.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo wakati akifungua semina ya maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi mkoani hapa juzi jioni. Alisema vurugu ni aina mpya ya uhalifu ambao umejitokeza hivi sasa na kulitaka jeshi hilo kujipanga kukabiliana nao.
“Pengine katika vyuo vya polisi hili halikuwa jambo kubwa, lakini sasa lazima iwepo mitaala hii, lazima mjaribu kulitazama,” alisema.
Alisema hayo ni mazingira mapya nchini na kwamba ni lazima kujenga uwezo wa kukabiliana nayo.
Alisema jambo la muhimu ni kuelekeza nguvu katika kuzuia vurugu zisitokee nchini. Kuhusu suala la maandamano, Rais Kikwete alilitaka jeshi hilo kutokuwa legevu katika kushughulikia maandamano ambayo yanaweza kuwa chanzo cha vurugu.
“Lakini msiwe na ulegevu, maana mkiwa na ulegevu nayo tutapata shida sana, itakuwa ni nchi ambayo haina utaratibu, ni haki ya watu kuandamana, lakini mkubali kuelekezwa mfanyeje ili mnapofanya hivyo msiharibu na haki za wengine,” alisema.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, alisema mwaka huu jeshi lake limeanzisha mkakati maalum wa kupunguza uhalifu ambao utaanzia katika ngazi ya taifa hadi katika ngazi ya kaya.
Aidha, alisema katika utekelezaji wa mpango huo, wamepanga mkakati na kuwa kila kamanda analazimika kusaini mkataba wa utendaji wa mwaka mmoja na IGP.
“Unalenga katika kupima ufanisi, kwa kutumia shabaha zilizowekwa katika maeneo manne katika eneo la kwanza kamanda anawajibika kuzuia uhalifu, vurugu na majanga katika himaya aliyokabidhiwa,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment