ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 14, 2013

KANDAMBILI ZASABABISHA KIFO CHA MWANAMKE MKOANI MARA.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa mara japhet lusingu akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
MAUAJI ya kikatili kwa wanawake mkoani Mara, yameendelea kushika kasi ambapo wanawake watatu wameuawa katika matukio yaliyotokea mfululizo kwa siku moja. 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Japhet Lusingu, alisema katika tukio la kwanza, mkazi wa Kijiji cha Tonyo, Kata ya Bisumwa wilayani Butiama, Happyness Lucas (25) alifariki dunia Februari 11, 2013 baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa teke tumboni na mume wake, Rugera John (27).
Chanzo cha ugomvi huo kilichosababisha kifo cha Happyness ni kugombea kandambili ambazo mume wa marehemu alikuwa amemnunulia mke mdogo.
Alisema baada ya kupigwa alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama kwa matibabu, ambapo saa tano usiku alifikwa na mauti.

Katika tukio jingine, alisema lilihusisha kifo cha mkazi wa Mtaa wa Chiringe wilayani Bunda, Rhobi Lucas (24), kilichotokea Februari 11, 2013 baada ya kushambuliwa na kupigwa mateke na mumewe, Masumbuko Khamis.

Alisema Januari 28, saa tatu usiku, Masumbuko alifika nyumbani kwake akiwa ameongozana na hawara yake na kuanzisha ugomvi baina yake na mkewe Rhobi, ambapo walianza kumshambulia marehemu kwa kushirikiana na mpenzi wake mwingine.

Alisema Rhobi aliamua kuondoka baada ya ugomvi huo na kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi na baadaye alikwenda kwa wazazi wake ambapo Januari 30, 2013 mumewe naye alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kuwa ameshambuliwa na kujeruhiwa na mkewe.

Alisema Februari 9, 2013, Rhobi alizidiwa na hali yake kuwa mbaya kutokana na kipigo hicho na alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Bunda na kulazwa kwa ajili ya matibabu zaidi.

Alisema Rhobi alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu na mtuhumiwa amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa upelelezi zaidi.

Katika tukio la tatu, mkazi wa Kijiji cha Kabegi, Ziada Sasita (35), aliuawa Februari 11, 2013 kwa kunyongwa shingo na watu wasiojulikana katika eneo la Mkirira, Kata ya Etaro wilayani Butiama na wauwaji walitumia nguo ya marehemu kumnyonga hadi kufa.

Alisema mtu huyo alikuwa anatoka kwa mjomba wake eneo la Mkirira, alikokwenda kusalimia na wakati akirudi nyumbani kwake alikoolewa ndipo alipofikwa na mauti.

Alisema mwili wa marehemu haukukutwa na jeraha lolote ila ulikutwa ukiwa na mtandio shingoni mwake wakati ulimi wake ukiwa umetoka nje.

Alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi unaendelea.

No comments: