Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilithi Mahenge |
Udhaifu huo umebaini huku serikali ikiwa imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kufanikisha utatuzi wa kero kwa wananchi.
Kati ya vijiji 15 vilivyoingizwa katika programu hiyo, halmashauri ya Kilindi imetekeleza mradi mmoja katika kijiji cha Kikunde pekee, huku sababu za uchelewaji zikielezwa kuwa ni ukosefu wa Mhandisi wa Maji tangu wilaya hiyo ilipoanzishwa mwaka 2005. Hayo yalibainika kufuatia ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Maji Dk Binilithi Mahenge yenye lengo la kukagua miradi ya maji inayotekelezwa katika halmashauri za mkoa wa Tanga.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Daudi Mayeji, ilisema katika mwaka wa fedha wa 2011/2012, walianza ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika kijiji cha Kikunde kwa gharama ya Shilingi milioni 384.5.
Mayeji alisema ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kwamba mchakato wa ujenzi wa mradi mwingine kijijini Negero, upo katika hatua za utekelezaji.
Wakati huo huo, serikali imeanza mchakato wa utumiaji nishati ya mionzi ya jua katika miradi ya maji, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuifanya iwe endelevu.
Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilithi Mahenge, alisema hayo wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilindi, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa mkoani Tanga.
Dk Mahenge, alisema kwa kuanza mchakato huo unatarajiwa kutekelezwa katika vijiji 200 nchi nzima.
“Tunaamini kwa kutumia mionzi ya jua, miradi mingi ya maji itakuwa endelevu, kwani wananchi hawataingia gharama za umeme na kununua mafuta kwa ajili ya jenereta,”alisema.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment