Leo nataka kuzungumzia matatizo wanayokutana nayo wanawake wengi wanaozalishwa na kuachwa bila huduma yoyote. Wengi wamekuwa wakipoteza dira ya maisha, hasa wanafunzi ambao wanapobeba ujauzito, husababisha kukatisha masomo na kuwa mwanzo wa kuyumba kimaisha.
Wapo ambao hukutana na mwanaume kwenye safari au kwenye mahafari yoyote na kujikuta wakishiriki tendo la ndoa bila kinga wakati hawajuani historia, wakati mwingine mwanamke anakuwa katika siku za hatari za kubeba ujauzito. Inawezekana kabisa ulikuwa kwenye starehe ya muda mfupi lakini baada ya kuachana unajikuta umeshika ujauzito.
Mnapoachana na mwenzako ambaye hamkupanga kuzaa zaidi ya starehe, hata ukimuona au ukimpigia simu anaweza akakutosa kwa vile hakujiandaa kuzaa na wewe.
Ingawa kwa upande mwingine inashangaza! Mtu anapokutana na msichana bila kutumia kinga anategemea nini, kama siyo kupata gonjwa la zinaa au
kumuachia ujauzito?
Huwa sikubaliani na mtu aliyekutana kimwili na mwanamke bila kinga, kuruka futi mia anapoelezwa amempa ujauzito mwenzake.
Napenda kuwatahadharidha wasichana wengi ambao ndiyo wapo kwenye janga la maambukizi au kubeba ujauzito kabla ya wakati, kwamba wanatakiwa wawe na uamuzi sahihi, hasa wa kukataa kitu ambacho wanaona kina madhara kwao.
Wengi wamejikuta wakiingia katika mapenzi kwa tamaa ya vitu kama fedha na simu ambazo hutumiwa na wanaume wakwale wanaoamini ile ndiyo njia ya kuwanasa wasichana ambao wamejiingiza katika dunia ya kisasa ya mtandao wa mawasiliano.
Niliishaelezea huko nyuma madhara ya simu kwa wasichana wadogo, hasa wanafunzi wanaotumia muda mwingi kuchati na marafiki kwenye BBM, Facebook, Twitter. Vitu hivi vimekuwa ndiyo chanzo cha wasichana wengi kujiingiza katika uhusiano na kusababisha kupata ujauzito na mwisho wake kuacha masomo na kuwa chanzo cha kupoteza dira ya maisha.
Tatizo kama hili halipo kwa wanafunzi au wasichana wadogo tu, bali limewakumba wanawake wengi, kiasi cha kufikia hatua ya kuongezeka kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Hili si tatizo la kujaa tu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, bali kuongezeka kwa wanawake wanaoishi maisha ya kubahatisha na mwisho wake kuangukia kwenye ukahaba kwa vile hana kazi, ana mtoto mdogo na aliyempa mimba hakubaliani naye kwa vile hawakupanga au alikuwa ni mume wa mtu.
Hali hii inaweza kuepukika kama mtu atajitambua kwa kujipangia maisha yake na kujua muda gani unamfaa kupata mtoto na muda gani si sahihi. Hata kwa wanafunzi nao wanatakiwa kutambua muda wa masomo ni wa masomo, mapenzi baadaye.
Umeshaanza mapenzi, utajilindaje?
Kama una uhusiano na mtu ambaye hamna malengo naye, usikubali kubeba mimba. Mtoto mara nyingi hutafutwa kwenye ndoa kwa vile wanandoa wana malengo ya kuishi kwa muda mrefu. Kwa vile una rafiki na ni lazima mkutane kimwili, basi tumieni kondomu. Si kwa kujikinga tu na Ukimwi, bali kujijengea misingi imara ya maisha.
Kwa kujitambua, wote wenye malengo katika maisha yao wajue kuzaa kwa bahati mbaya si dhambi. Lakini lazima watambue kubeba mimba bila kupanga si fasheni bali kujiingiza kwenye matatizo yasiyo ya lazima.
Tumia tarehe za mzunguko wa hedhi ili kujikinga na mimba zisizotegemewa, kama hujui tumia kondomu, hivi vyote ukivifuata vitakufanya uwe salama.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment