ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 18, 2013

MAUAJI YA PADRI RAIS SHEIN ATOA MKONO WA RAMBIRAMBI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mjini Unguja kwa niaba ya Dk Shein ambaye alitumwa kwenda kuonana na familia ya Padri Muchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mjini Unguja kwa niaba ya Dk Shein ambaye alitumwa kwenda kuonana na familia ya Padri Muchi.
Na SALMA SAID
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein amewataka waumini wa dini ya kikristo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha msiba kufuatia kifo cha Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar kilichotokea juzi Beit El Raas Mjini Unguja.
Salamu hizo zimetolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mjini Unguja kwa niaba ya Dk Shein ambaye alitumwa kwenda kuonana na familia ya Padri Muchi.
Aboud amesema Rais Kikwete na Rais Shein wote hawapendi kusikia na kuona vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani vikitokea katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania na kutokana na sababu hizo wameomba msaada kwa nchi nyengine zenye ujuzi wa masuala kama hayo kuja kufanya utafiti wa kuwabaini wahusika wenye kuendesha vitendo hivyo.
Dkt Shein jana alikutana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Minara Miwili, Augostine Shao huko katika Ikulu ndogo Migombani na kueleza masikitiko yake kutokana na kifo hicho cha hafla cha Padri Evarist Muchi wa Kanisa Katoliki la Zanzibar, na kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.
Katika mazungumzo na Waandishi wa Habari,  Waziri Aboud alisema kuwa Serikali imejipanga vizuri  kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa mara moja.
“Kutona na jiografia ya Zanzibar, Tunaelewa kwamba zipo sehemu katika kisiwa cha Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili kupambana na uhalifu “, alisema Aboud.
Alisema matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya usiri mkubwa kwa hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa mashirikiano  kwa Jeshi la Polisi pale wanapohitajika.
Akizungumzia suala la bandari bubu kuwepo Zanzibar ambazo zinapitisha silaha ovyo, Aboud alikiri kuwepo kwa bandari hizo na kusema kwamba kutokana na mazingira ya Zanzibar kuwa kisiwa bandari hizo haziwezi kukosekana lakini aliahidi serikali kuongeza ulinzi katika maeneo yote hayo.
Aidha alisema alikanusha taarifa zilizozagaa mitaani za kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na kuwataka wananchi kuondoa khofu hiyo.
“Zanzibar ni kisiwa, na kwenye kisiwa bandari kama hizo zisizo rasmi haziwezi kukosekana na hilo la kuingizwa silaha tunalifahamu lakini bado tunasema kwamba tutaongeza nguvu ya kuweka ulinzi katika bandari hizo ili kudhibiti mambo kama hayo yanayohatarisha katika nchi yetu” aliongeza Aboud.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Zanzibar mtu kuwa na silaha ni kosa la jinai na hivyo kuwaomba wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi wanapopata taarifa za kuwafahamu watu wenye silaha mitaani ambazo mwisho wake hutumika katika kuwahujumu watu wengine.
Sambamba na hayo, Aboud amewataka viongozi wa dini mbali mbali  pamoja na waumini wa dini zote  hapa Zanzibar kuwa  wastamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi. Aidha, Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa waumini wa dini zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa na migongano ya kidini.
Waziri huyo alikanusha kuwa wachunguzi kutoka nje kuja Zanzibar kutawatia khofu wananchi bali alisema ni kwa sababu ya kuongeza nguvu kwa ulinzi.
“Kuwaomba walinzi kutoka nje nio kuwatia khofu wananchi lakini ni kutaka kuongeza nguvu kwa vyombo vyetu vya serikali kwa sababu wenzetu wana uzoefu mkubwa wa masuala hayo” alisema Aboud.
Aliwaambia waandishi wa habari kwamba zipo kasoro kwa jeshi la polisi lakini pia wamekuwa wakifanya kazi vizuri na kuwataka wananchi kuwaunga mkono kwa kuwasaidia kuwafichua wahalifu ambao wanaonekana kuendeleza matukio kama hayo ya kihalifu.
Aboud alisema mtandao wa matukio hayo ni mkubwa na unapaswa kuvunjwa lakini wananchi wasiposhirikiana na serikali kwa kutoa taarifa kwa jehsi la polisi kazi hiyo itakuwa ni ngumu kufanikiwa.
“Tunataka kumaliza huu mtandao kwa hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa vyombo vyetu vya ulinzi ili kufanikisha hili suala bila ya mashirikiano matumaini ya kuwamaliza wahalifu itakuwa ni vigumu” alisema.
Akijibu masuali ya waandishi wa habari kuhusiana na kuchelewa kutolewa ripoti ya uchunguzi wa matukio ya uhalifu yaliotangulia huenda ndio yaliochangia kusababisha tukio hilo la mauaji kutokana na wananchi kukata tamaa, Aboud alisema inawezekana kuchelewa huko kumechangia kwa kiasi fulani lakini akasema uchunguzi wowote unahitaji muda wa kutosha ili kujua chanzo cha tatizo kabla ya kuwasilishwa ripoti kamili.

No comments: