Ustadhi Yahya Michael, mkazi wa Dar, hivi karibuni amejitokeza na kudai kuwa yeye ndiye mganga aliyempaisha mwanamuziki Nasibu Abdu ‘Diamond Platnumz’ ambaye kwa sasa ni kinara wa Bongo Fleva, Risasi Jumamosi lina mkanda kamili.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum maeneo ya Magomeni, Dar, mganga huyo alidai kuwa pamoja na jitihada kubwa alizofanya kumpaisha Diamond lakini anamshangaa kwa kuwa amesahau alikotoka na anajifanya supastaa.
Alidai kuwa siku hizi akimpigia simu, Diamond huwa hapokei, tofauti na zamani alipokuwa akihangaika kuchomoka kisanii.
Mganga huyo alifunguka kuwa sababu ya kufanya hivyo ni baada ya kuchukuliwa na watu waliompeleka kwa waganga wa Kigoma ambako anajidanganya kuwa ndiyo wanampaisha kumbe walimchukua akiwa ameshampandisha kwa kumpa dawa kali za mvuto.
ALIMPA DAWA GANI?
Alizitaja dawa alizompatia Diamond kuwa ni mitishamba aina ya Dubi, Ntajamasala (hii humfanya watu wamuogope na kumheshimu), Italigula, Nkangacharo na Kalila Lila (ambayo huichoma na kuoga kwa ajili ya kuwavutia watu).
ANGUKO LA DIAMOND
Alidai kuwa Diamond amejisahau na hajui kama anguko lake linakuja kufuatia ahadi aliyoiweka wakati anaanza kuimba baada ya kumpatia dawa hivyo atapotea kwenye muziki.
Akielezea historia ya kukutana kwao, Ustadhi Yahya alisema yeye na staa huyo walikutana miaka ya 2000 nyumbani kwa Papaa Misifa ambaye alikuwa meneja wa Diamond.
Alidai kuwa kubadilika kwa Diamond kulikuja baada ya kutwaa tuzo tatu za Kili mwaka 2010 ndipo akawa anahusudu wanawake tofauti na masharti ya dawa japokuwa alimkanya lakini hakumsikia.
DIAMOND ANASEMAJE?
Kama ilivyo desturi ya gazeti hili, lilimgeukia Diamond ili kupata mzani wa habari hiyo ambapo alipopatikana kwa njia ya simu alisomewa maelezo yake yote.
AMKANA
Katika maelezo yake, Diamond alikataa kata kata kuwa hamfahamu mtu huyo kisha akakata simu.
“Sina msikiti nitakuwaje na Ustadhi? Huyo mganga nasema simfahamu,” alisema kisha akakata simu.
1 comment:
Tulijuwa tu, wasanii wa bongofleva wnalazimisha vipaji. Diamond ni mwanamuziki?
Post a Comment