ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 7, 2013

Msuya alazwa Hospitali ya Moi

WAZIRI Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amelazwa katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi).

Msuya mwenye umri wa miaka 83, alifikishwa hospitalini hapo kwa matibabu Februari 4, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi. Mwanasiasa huyo mkongwe amelazwa kwenye vyumba vya sehemu ya kulipia vya hospitali hiyo.


Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Moi, Almas Jumaa alithibitisha kupokelewa kwa Msuya na kudai kuwa bado anaendelea na matibabu.
“Ni kweli tumempokea Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya tangu Februari 4, mwaka huu, yupo chini ya uangalizi maalumu kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Jumaa.

Jumaa alisema Msuya, ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mwanga, anashughulikiwa na jopo la madaktari bingwa kutoka Muhimbili na Moi ili waweze kujua maradhi yanayomsumbua.
Jumaa alisema kuwa kwa sasa hali yake inaendelea vizuri ikilinganishwa na kipindi alichofikishwa na kwamba madaktari wanaendelea na uchunguzi zaidi.

Msuya, ambaye alizaliwa Novemba 4, 1931, ni kati ya wanasiasa maarufu nchini kutokana na kuwahi kuwa Waziri Mkuu katika vipindi viwili tofauti.

Mara ya kwanza alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1980 hadi 1983 wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza wa Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.

Pia aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mwaka 1994 hadi 1995 wakati wa utawala wa Awamu ya Pili uliokuwa chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Msuya, ambaye aliitumikia Serikali kwa muda mrefu kuanzia kipindi cha ukoloni hadi Tanzania ilipokuwa huru alipomaliza Chuo Kikuu cha Makerere huko Uganda, pia aliwahi kuwa Waziri wa Fedha, pia Viwanda.
Kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara za Ardhi, Fedha, Maji na ile ya Utamaduni na Ustawi wa Jamii.
Mwananchi


No comments: