Friday, February 8, 2013

Msuya apelekwa Uingereza kutibiwa

Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, aliyekuwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI), amepelekwa nchini Uingereza kwa matibabu zaidi.
Afisa Habari wa Taasisi hiyo, Jumaa Almasi, alisema jana kuwa Mzee Msuya aliondolewa MOI juzi saa 3:00 usiku.

“Serikali imeamua kumpeleka Mzee Msuya nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi, na aliondolewa hospitalini hapa jana (juzi) usiku,” alisema Almasi.

Hata hivyo, bado haijaeleweka ugonjwa unaomsumbua kiongozi huyo mstaafu. Serikali na Moi hawakuwa tayari kuzungumzia igonjwa unaomsumbua.

NIPASHE jana ilimtafuta Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, DK Hussein Mwinyi, ambaye licha ya kuthibitisha kuwa na taarifa za kupelekwa nchini Uingereza kwa Mzee Msuya, lakini hakutaka kuweka wazi ugonjwa unaomsumbua.

Mzee Msuya alilazwa kitengo cha mifupa tangu Jumatatu wiki hii na kuwekwa chini ya uangalizi wa jopo la madaktari wa taasisi hiyo pamoja na wenzao wa Muhimbili, ambao walikuwa wanamfanyia uchunguzi wa afya yake na ilielezwa kuwa hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.

Mzee Msuya alikuwa Waziri Mkuu kwenye uongozi wa awamu ya kwanza ya Hayati Mwalimu Jullius Nyerere, na awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi .

Mbali na uwaziri mkuu, Msuya ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga kwa muda mrefu, alishika nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo uwaziri katika wizara mbalimbali katika awamu ya kwanza na pili.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake