Saturday, February 2, 2013

Mtoto mlemavu wa ngozi (albino) kukatwa mkono

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Antony Rutta
Mtoto Lugolola Bunzari (7) mlemavu wa ngozi (albino) amepoteza maisha baada ya kukatwa mkono na kuvuja damu nyingi, kwenye tukio lililotokea wiki hii mkoani Tabora.

Kadhalika babu wa mtoto huyo aliuawa wakati akijaribu kumuokoa mjukuu wake baada ya kushambuliwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na kuvuja damu nyingi.

Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Antony Rutta, alisema mtoto huyo alikatwa mkono wa kushoto na mauaji hayo yalitokea juzi saa 10 alfajiri katika kitongoji cha Kinondoni kilichoko kijiji cha Kanoge wilayani Kaliua mkoani humo.

Akizungumza na waadishi wa habari alisema watu nane ambao hawajafahamika wakiwa na gobore, mapanga na marungu walivamia nyumbani kwa Bunzari Shinga (33) baba wa mtoto huyo, kuishambulia familia yake kabla ya kumkamata mtoto huyo na kumkata mkono walioondoka nao.Alisema pamoja na kumkata mkono mtoto huyo walimpiga mapanga Zengabuyaga Meli (95) babu wa mtoto huyo aliyejaribu kumsaadia mjukuu wake asiuliwe.
Meli aliyekatwa mkono wa kulia , kichwani na begani alivuja damu nyingi na kufariki dunia muda mfupi baadaye.

Aidha Kamanda Rutta alisema licha ya watu hao kusababisha vifo vya watu hao pia waliwajeruhi baba wa mtoto huyo Shinga kwa kumpiga risasi mguu wa kulia ambapo alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Kitete mjini hapa .

Pia Kamanda alisema walimjeruhi Dama Buyaga bibi wa albino huyo na sasa amelazwa Kitete na hali yake inaelezwa kuwa hairidhishi.

Alihusisha mauji hayo na imani za kishirikina na kwamba uchuguzi unaendelea na kuongeza kuwa mauaji hayo ya albino ni ya kwanza mkoa humo.

Alisema familia ya Shinga inaishi porini hivyo ilikuwa vigumu kupata msaada kutoka kwa majirani. Kamada Rutta alitoa wito kwa wananchi na raia wema kushirikiana na polisi kuwabaini na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: