Saturday, February 2, 2013

Gesi ya Mtwara yawaka bungeni

Kiongozi wa kambi ya upinzani, Freeman Mbowe
*Mbowe ataka waliosababisha vurugu Mtwara wawajibishwe
*Pinda asema hilo liko chini ya ofisi yake na ofisi ya Rais

VURUGU zilizofanywa na wananchi wa Mtwara, wakipinga mitambo ya kusafirisha gesi kujengwa Dar es Salaam, zimewasha moto bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kuhoji ni hatua gani watakazochukuliwa viongozi waliosababisha vurugu hizo. Mbowe alimuuliza swali hilo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni wananchi wa Mtwara, wameandamana na kusababisha uharibifu wa mali kwa sababu ya kupinga mitambo ya gesi isijengwe Dar es Salaam bali ijengwe Mtwara.

“Je ni hatua gani Serikali itawachukulia watendaji wake na vyombo vya usalama, kwa kushindwa kuzuia na kudhibiti vurugu hizo.

“Na pia kama kweli Serikali ni sikivu, kwa nini ilisubiri muda mwingi upite bila kuchukua hatua mapema?” alihoji Mbowe.Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema suala hilo liko chini ya uwezo wa ofisi yake pamoja na Ofisi ya Rais na kwamba, wataangalia namna ya kulifanyia kazi.

“Suala hili liko ndani ya uwezo wa ofisi yangu pamoja na Rais, kwa hiyo tutaangalia namna ya kulishughulikia.

“Lakini hapa naona Mbowe anajenga hoja isiyo na mashiko, suluhu ya jambo hili haikuwa maandamano na isingefikiwa kwa maandamano.

“Mzozo wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, ulichangiwa kwa asilimia kubwa na upotoshaji uliofanywa na vyama vyote vya siasa kwa ujumla wake.

“Serikali siku zote imekuwa sikivu na itaendelea kupokea ushauri wowote utakaolenga maendeleo ya nchi na kulinda amani na utulivu.

“Serikali imekuwa sikivu muda wote na tutaendelea kuwa wasikivu pale tunapoona jambo husika lina tija kwa taifa,” alisema Pinda.

Awali Mbowe alitaka kujua ni kwa nini mikataba yote inayoingiwa na Serikali isiwekwe wazi kwa kuwa kitendo cha kuifanya siri, ndiyo chanzo cha vurugu kama zilizotokea Mtwara.

Kwa mujibu wa Mbowe, kutokuwekwa wazi mikataba hiyo ndiyo sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi kwa sababu hawajui kilichoridhiwa na Serikali.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali haimzuii mwananchi yeyote kujua mikataba hiyo ilivyo na kwamba, kama Mbowe anaitaka anatakiwa kufuata utaratibu.

“Hakuna anayemnyima mwananchi mkataba anaotaka kujua. Katika hili ni vema wabunge mkafuata taratibu za kuipata kwa kupitia Ofisi ya Spika wa Bunge, ili muisome na muielewe na kisha mpeleke mrejesho kwa wananchi wenu bila kupotosha ukweli.

Pinda alisema, mzozo wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, ulichangiwa kwa asilimia kubwa na vyama vyote vya siasa kwa ujumla wake, kwa kupotosha ukweli.

Alisema, Serikali siku zote imekuwa sikivu na itaendelea kupokea ushauri wowote utakaolenga maendeleo ya nchi na kulinda amani na utulivu.

Wiki iliyopita, wananchi wa mjini Mtwara, walifanya vurugu na kuharibu baadhi ya mali ikiwamo nyumba ya Waziri wa TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM).

Pia wananchi hao walichoma Mahakama na Mwanzo Mtwara na kuharibu pia nyumba za viongozi kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mtwara.

Mbali na vurugu hizo, zingine zilifanyika mjini Masasi ambako wananchi walichoma moto nyumba ya Mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe (CCM) pamoja na nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM).

Pia wananchi hao walichoma moto magari ya Serikali, magari ya watu binafsi pamoja na jengo la Mahakama ya Mwanzo na kituo cha polisi mjini humo.

Kutokana na vurugu hizo, Waziri Mkuu Pinda akiwa na viongozi kadhaa wa Serikali, alikwenda mkoani humo ambako alikutana na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuangalia namna ya kutatua malalamiko yao.

Alipomaliza kukutana na makundi hayo, juzi Waziri Mkuu alikutana na wabunge mjini Dodoma na kuwaleza kwa kina alichojionea Mtwara jambo ambalo lililifanya Bunge lisitishe mpango wake wa kuunda tume liliyokuwa limepanga kuunda ili kufuatilia vurugu hizo.

No comments: