Advertisements

Sunday, February 24, 2013

Padri Mushi azidi kuwaliza Wakatoliki

Serikali imetakiwa kutolichukulia kwa wepesi mauaji ya viongozi wa dini yanayoongezeka, badala yake ichukue hatua kwa vitendo.

Paroko wa Parokia ya Mawela wilayani Moshi, Anthony Marunda, alitoa angalizo hilo alipozungumza na NIPASHE Jumapili, iliyotaka kupata maoni yake kuhusiana na mauaji ya Padri Evaristus Mushi, aliyeuawa Jumapili iliyopita Visiwani Zanzibar.

Mawela ni parokia mama ya nyumbani kwao marehemu Padri Mushi, ambako Padri Marunda, alisema kwa sasa watu wameshikwa na hofu na kuwauliza viongozi wao wa kiroho juu ya jambo gani linapaswa kufanywa kipindi hiki cha Kwaresma.

“Zipo kila alama za kuonyesha amani inatoweka, kanisa linakemea kwa nguvu tukio hilo ambalo limetoa taswira ya viongozi wa dini kuuawa, tunaitaka serikali kufikiria la kufanya ambalo litakuwa suluhisho la kudumu,” alisema.

Alisema marehemu Padri Mushi, alikuwa mwenye msimamo, asiye na woga katika kukemea uovu au yasiyostahili kwenye jamii.
“Hivyo hata kama ameuawa, lakini ametimiza wajibu wake kwa kuwapa mafundisho yanayopaswa kutolewa kwa jamii yake aliyokuwa anaiongoza,” alisema.

Alisema waliwahi kufanya kazi pamoja katika parokia ya Kipalapala, wakati marehemu Padri Mushi akiwa Shemasi, lakini (Mushi) alionyesha ujasiri wa kuwa na msimamo wa kupinga uovu kwenye jamii na kusimama katika haki na usawa.

“Inashtusha na kutia hofu, lakini bado haitukatishi tamaa kama viongozi wa dini, tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuieleza jamii juu ya mambo ambayo hayastahili,” alisema.

Aliongeza, “kazi yetu si kuwafurahisha wanadamu, bali Mungu pekee na tunafanya kazi ya utume ambayo ndiyo ametutuma.”

Mmoja wa majirani wa karibu wa nyumbani kwao marehemu Padri Mushi, John Mushi, alisema maisha ya marehemu (wakati wa uhai wake) yalikuwa visiwani Zanzibar kuliko mahali alipozaliwa, Kilimanjaro.

Alisema matukio ya hujuma na mauaji yanayowahusisha viongozi wa dini, yataliangamiza taifa kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa katika kuyadhibiti. “Tunaekelea kubaya sana, taifa linapinduka na kuharibika mikononi mwetu, katika umri wangu sijawahi kuona matendo kama hayo, watu wamekosa uvumilivu,” alisema.

NIPASHE ilifika nyumbani alikozaliwa Padri Mushi, na kukuta watu mbalimbali wakiwa kwenye majozi, huku wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kutoka Zanzibar.

Wakati mwili wa Padri Mushi ukilazwa kaburini na kuonekana kupitia runinga, wakazi hao kutoka madhehebu tofauti walibubujikwa machozi wakionyesha kusononeka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: