ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 24, 2013

Pinda amuunga mkono Lowassa

Mh. Mizengo Pinda
 *Aunda tume kuchunguza matokeo kidato cha nne
*IGP Mwema: Waliofeli mitihani watachochea uhalifu nchini
*Mwakyembe: Mafisadi wanaathiri uboreshaji huduma za jamii


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameunda tume maalum itakayofanya uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka 2012, yakihusisha kiwango duni cha ufaulu.

Matokeo hayo yalitangazwa hivi karibuni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, huku idadi kubwa ya wanafunzi (takribani asilimia 60) wakishindwa kwa kupata daraja sifuri.

Hali hiyo imeibua shinikizo kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali,  wakiielekezea kidole serikali kwa kile kinachoaminika kuwa ni kushindwa kuiboresha sekta ya elimu, huku wengine wakitaka viongozi wa wizara hiyo akiwamo Dk. Kawambwa, kujiuzulu.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa, tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi wiki ijayo.
Kwa mujibu wa Lyimo, wajumbe wake watatoka Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi, (TAMONGSCO), taasisi za dini zinazotoa huduma ya elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazoshughulikia masuala ya elimu.

Wadau wengine watakaoshiriki ni Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).

Lyimo alisema serikali inawaomba wadau wa elimu, wazazi, walezi na wananchi wote kwa ujumla watoe ushirikiano kwa tume ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Hatua ya Pinda imekuja siku mbili baada ya mtangulizi wake, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutoa rai ya kuundwa tume itakayochunguza sakata hilo kwa lengo la kuinusuru sekta ya elimu nchini. Lowassa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii kuwa, kufeli kwa wanafunzi katika kiwango kikubwa kiasi hicho ni aibu, hivyo pamoja na mambo mengine, ipo haja ya kuundwa tume mahususi kwa ajili ya suala hilo.

Kwa msisitizo alisema; “Matokeo ya kidato cha nne yamenishtua sana. Ninamuomba Rais kama ambavyo amefanikiwa katika sekta nyingine, aunde tume ya kitaifa kuchunguza suala la elimu kutoka kwa wadau mbalimbali nchini. Wakati umefika Tuache kuoneana haya suala hili.

“Ni lazima iundwe tume ili itusaidie kutuletea matokeo yanayosababisha tatizo hili kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi zaidi Bila hivyo tutakuwa tunaliumiza taifa na pia tunajenga kizazi cha mazezeta ambacho kitashindwa hata kushindana na soko la Afrika mashariki…”.

MWAKYEMBE ALIA NA MAFISADI
Wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema kushamiri kwa viongozi mafisadi wanaopora rasilimali za umma, kumechangia kufifisha jitihada za kuboresha sekta muhimu kwa ustawi wa jamii ikiwamo elimu.

Dk. Mwakyembe alisema atapigana hadi tone la mwisho, kuhakikisha mkakati wa kuwatokomeza mafisadi waliomo ndani na nje ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wanashindwa, hivyo kutoa mwanya wa kupiga hatua za maendeleo.

Alikuwa akizungumza kwa niaba ya wazazi katika mahafali ya pili ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam jana.

Dk. Mwakyembe aliwataka wananchi wasimlaumu Rais Kikwete, kwani hata yeye inafikia wakati anajikuta anashindwa kuchukua hatua kutokana na nguvu kubwa walizonazo mafisadi hao.

Alisema nchi ilipofikia, imekuwa ikiliwa na watu wachache ambapo matokeo yake hata sekta muhimu kama elimu inazidi kudidimia kwa kukosa fedha za kuhudumia shule za serikali. "Nawaombeni wananchi msimlaumu Rais Kikwete, miongoni mwa viongozi wanamuangusha, inafikia kipindi anabaki hana la kufanya kwa sababu tuliokabidhiwa mamlaka, wapo wanaokula kila kitu na kuiacha nchi ikiwa tupu," alisema.

"Rasilimali ni zenu ninyi vijana, hakuna atakayethubutu kuzila, tutahakikisha utamaduni huu wa kipuuzi kabisa tunautokomeza," alisema.

Hata hivyo, aliwataka wahitimu hao kuhakikisha wanaendelea na masomo ya juu waweze kukabiliana na soko la ushindani hususani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema tabia ya vijana kupenda vitu vya anasa vimepitwa na wakati, kwa kuwa dunia inabadilika kwa kila nchi kuhakikisha inapata watu wenye elimu ya kutosha kwa ajili ya kukuza maendeleo na sio vinginevyo. Awali Mkuu wa shule hiyo, Mtawa Theidora Faustine alisema jumla ya wanafunzi 194 wamemaliza masomo hayo wakiwamo wasichana 64 na wavulana 130.

IGP MWEMA AHOFIA ONGEZEKO LA UHALIFU
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, amesema kama taifa litashindwa kuiboresha sekta ya elimu, kuna hatari kwa nchi kukabiliwa na ongezeko la vitendo vya uhalifu.

IGP Mwema alisema hayo kwenye hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Kamishna wa Polisi, Clodwig Mtweve, kwenye mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Lord Baden Powell ya jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mshtuko mkubwa uliotokea katika sekta ya elimu unaweza kusababisha vijana wengi kuingia mitaani, hivyo baadhi yao wanaweza kujihusisha na matukio ya uhalifu.

Mkuu wa Shule ya Lord Baden, Iddi Kipingu, alisema ipo haja ya ushiriki wa kada zote kushiriki katika kuwalinda na kuwalea watoto, kama moja ya njia za kuwawezesha kufaulu vizuri katika masomo yao.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

The reactive nation. They always react after the fact. Tume ya nini sasa? Unataka kuniambia kuwa hakuna studies ambazo zimeisha ainisha jinsi ya kuboresha elimu nchini? This is misallocation of resources. I do not agree with the idea. NO.

Let me hear what do you think?