Ernest Mangu |
Mwili wa Alfred unatarajiwa kusafirishwa leo kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kidaktari ili kujua sababu hasa za kifo chake.
Baba mzazi wa marehemu, Fred Mallya, aliliambia NIPASHE jana kuwa taratibu zote za kusafirisha mwili zimekamilika isipokuwa walikuwa wanasubiri madaktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi huo. “Tulikubaliana na Jeshi la Polisi kwamba mwili wa mwanangu ufanyiwe uchunguzi kwanza ili tujue kilichosababisha kifo chake ndipo twende Moshi kwa mazishi. Lakini ikaonekana madaktari wa kufanya postmortem (uchunguzi wa kidaktari) wa hapa Bugando wamesafiri.
Hivyo, tukakubaliana tuwasubiri hadi Jumatatu ijayo watakapokuwa wamerudi,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya kushauriana na maofisa wa polisi, akiwamo ndugu wa karibu, ambaye pia ni ofisa wa polisi aliyeko Dar es Salaam, walikubaliana na ushauri wa Jeshi la Polisi wa kuwaleta madaktari wengine kutoka MNH ili waende kuufanyia uchunguzi mwili huo.
Mallya alisema hadi sasa anaendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Jeshi la Polisi jijini Mwanza na kwamba, wamekubali kulipia gharama za matibabu, kununua jeneza pamoja na kukodi gari la kusafirisha maiti kwenda Moshi.
Kuhusu hatua gani ambayo anatarajia kuichukua dhidi ya askari anayedaiwa kumpiga mwanaye na kusababisha kifo chake, Mallya alisema suala hilo litajulikana baada ya kumaliza shughuli za mazishi, lakini akadokeza ni lazima atakwenda mahakamani.
“Wao (polisi) wanadai askari anayedaiwa kumsababishia kifo mwanangu eti ametoroka. Ila kama watamkamata niko tayari kusimama naye mahakamani. Lakini kama hatapatikana, nitalishtaki Jeshi la Polisi,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, amekuwa akikwepa kuzungumzia tukio hilo.
NIPASHE ilijaribu kuwasiliana naye kwa siku tatu mfululizo, lakini amekuwa akitoa majibu yasiyoridhisha.
Jumatatu iliyopita, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alidai hajapata taarifa kwa sababu alikuwa ndiyo kwanza amefika Mwanza akitokea safarini mkoani Dodoma.
Alipotafutwa tena juzi, alidai alikuwa ndiyo ameingia ofisini, hivyo atafuatilia na angetoa taarifa siku inayofuata.
Hata hivyo, jana alipopigiwa simu na kuulizwa iwapo ameshapata taarifa za tukio hilo, alidai yupo kwenye kikao na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) mkoani Mwanza.
Baadaye majira ya saa 11:00 jioni simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment