Friday, February 8, 2013

UHUSIANO WA DINI, KABILA, MILA KWENYE NDOA! – 2

MUNGU mtakatifu mwingi wa rehema, fadhili zako ni za milele. Sifa, heshima na utukufu navirejesha kwako kwakuwa wewe ndiye unayestahili.

Marafiki zangu wapendwa, wiki iliyopita nilianza kwa kugusia suala la umuhimu wa wanandoa kuwa na imani moja, maana imani ya dini ndiyo msingi wa maisha.

Hofu, adabu na maisha yenye mwongozo sahihi juu ya Mungu huanzia kwenye imani. Ni sahihi zaidi kuoana kwa dini moja. Pia nilielezea kuhusu mmoja kubadili dini na kumfuata mwenzake.
Hapo pia kuna tatizo, zipo athari nyingi ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kubadilisha imani yake ili aoe au kuolewa.

KWA NINI USIBADILI KAMA UMEMPENDA?
Hapa kwenye kubadili dini huwa na changamoto nyingi sana. Kwanza kunaweza kusababisha mgongano wa wazazi na mtoto – wakati mwingine hufikia hatua ya kutishia kulaaniwa.
Ndugu zangu, hatupaswi kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja. Upendo unabaki kuwa upendo na dini inabaki kuwa dini. Kubadilisha dini hakumaanishi unavyompenda mwenzako bali kunadhihirisha usivyo na msimamo na maisha yako.
Imani ya dini ndiyo dira, kubabaika ndani yake maana yake hata kwenye mapenzi utakuwa unakokotwa tu! Kuwa na msimamo. Simamia unachokiamini. Kama ulibadili dini kwa sababu ya imani kabla hamjakutana na ukaamua kuoana naye ni sawa na si kubadilisha dini ili uingie kwenye ndoa.NDOA YA MSETO
Siku hizi kuna utaratibu wa ndoa za mseto; baadhi ya madhehebu yanaruhusu maharusi waoane chini ya msimamo wa imani yao hata kama kila mmoja anaabudu kwake. Kisheria halina tatizo hasa kwa kuwa suala la ndoa ni la kisheria zaidi.
Tunaporudi katika utaratibu wa maisha ya kawaida ndipo tunapokutana na matatizo. Yapo matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea kwa kuishi wanandoa wawili huku kila mmoja akiwa na imani yake. Nilieleza kwa uchache sana hapo juu, lakini hapa nitafafanua zaidi.

USULUHISHI WA MASHAKA
Kama nilivyotangulia kusema kwamba imani ndiyo msingi, hivyo hata katika uhusiano na ndoa migogoro ikizidi, njia salama na za siri zaidi kumaliza ukiondoa kwa wanasaikolojia ni katika imani za dini. Tafiti zinaonesha kwamba, kesi nyingi zinazopelekwa kwa viongozi wa dini huisha kwa amani kuliko zile za kisheria.
Kuwa na imani tofauti, maana yake wanandoa wanakosa mahali sahihi pa kupeleka matatizo yao. Upo ushahidi mwingi wa wazi juu ya matatizo haya. Kabla sijaenda mbele zaidi, nitakupa ushuhuda wa wasomaji wawili niliowasiliana nao wiki iliyopita.
Dk. Kilian Mlangwa (mshauri wa ndoa na uzazi na mkufunzi wa semina za ndoa) wa Dar es Salaam, aliposoma makala haya wiki iliyopita alinipigia simu na kueleza namna suala la dini na mila linavyogusa maisha ya wanandoa wengi.
“Ndugu yangu umepatia sana kwenye hii mada yako ya leo (Ijumaa iliyopita). Nimekutana na kesi nyingi za aina hii. Kuandika kwako gazetini kutasaidia elimu hii kuwafikia wengi kwa wakati mmoja,” alisema Dk. Mlangwa.
Msomaji mwingine ambaye alisema yeye ni mama mwenye umri wa miaka 45 (nahifadhi jina lake) alieleza namna uamuzi wake wa kubadilisha dini na kuolewa na mume wake unavyompa mateso makubwa kwenye ndoa yake hivi sasa.
Nilizungumza mengi sana na mama huyo, naamini aliyoniambia yanaweza kubadilisha mtazamo wa vijana wengi na kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa ambazo zinaweza kuwasababishia matatizo.
Kukosa ushuhuda wa mama huyo ni sawa na kujinyima ushahidi wa maisha sahihi yanayotokana na mwongozo chanya juu ya ndoa. Nakusihi sana rafiki yangu, USIKOSE!

GPL.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake