Na Flora Mwingia.
“Kuna familia zingine hazihitaji mikopo lakini utaona mwanamke analazimisha kujiunga na Vicoba. Mume akikataa mwanamke anajiunga kwa nguvu.Hii inapelekea kwenda kinyume na maagizo ya Muumba wetu kwamba mwanamke anapaswa kuwa mtii kwa mumewe. Matokeo yake nyumba inakuwa kwenye turmoil(vurugu). Kuna mke wa rafiki yangu alikopa Vicoba kwa siri akaweka rehani samani zote za nyumbani akawekeza kwenye mradi wa mitumba.
Aliposhindwa kurejesha Vicoba wakataka kupiga mnada samani ndipo mume akashtuka. Ilibidi mke asepe kusikojulikana. Ilibidi mwanaume aingie mkataba na Vikoba akalipa deni kwa miezi mitatu ndipo mama akarejea! (Mosoi).”
Msomaji huyu alituma ujumbe huo akihusisha na mada
Naam. Mambo ndio mambo. Ni hivi majuzi tu wakati nikiwa likizo nilibahatika kuzungumza na baadhi ya kinamama ambao wanafurahia mikopo ya Vicoba ingawa wengine wamekuwa wakikumbana na kashkash baada ya kushindwa kurejesa ipasavyo.
Wanasema kuwa mikopo hiyo imewasaidia sana katika kukabiliana na ugumu wa maisha na pia imekuwa changamoto kubwa kwao kutokana na jinsi wanavyojishughulisha ili waweze kurejesha kwa wakati.
“Mikopo hii imetusaidia sana. Tunamshukuru sana Mzee Reginald Mengi ambaye ndiyo aliyeanzisha utaratibu huu kutukomboa sisi wanawake. Mungu amzidishie pale anapotoa kwa ajili ya wahitaji kama sisi.
“Ila wapo baadhi yetu ambao wamekuwa wanaharibu utaratibu huu baada ya kupewa mikopo wanaacha kuitumia kwa lengo husika na badala yake kuzitumia kwa anasa. Matokeo yake wanashindwa kurejesha ili wengine nao wapate”, anasema mama Helena mkazi wa Mamsera, wilayani Rombo.
Mwingine, Mama Elia ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kiungu kijiji cha Mamsera Kati anasema’ “Mikopo hii ni mizuri sana. Kinamama hivi sasa wameamka kimaendeleo kwani imewasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi na nguruwe. Lakini wengine wameitumia vibaya na matokeo yake maofisa mikopo wanapowafuatilia wanakuta hawajafanya cha maana.
“Hawa ndio wale wanaojikuta wakichukuliwa mali zao kisha zikapigwa mnada kurudisha mikopo na pia kushitakiwa kwa kukiuka masharti ya mikopo. Hili siyo jambo zuri”, anamaliza kusema mwalimu huyu.
Wengine wamekuwa wakichukua mikopo hiyo bila kuwashirikisha wake au waume zao au jamaa zao. Kwa mfano, mzee John Shayo mkulima wa Mengwe, Rombo yeye anasema kuwa mikopo ni mizuri lakini inataka nidhamu ya hali ya juu. “Kama huna nidhamu huwezi kusimamia mkopo unufaike, badala yake utakuingiza kwenye matatizo makubwa”.
Anatoa mfano wa mkamwana wake(mke wa mwanae) ambaye alitimkia kusikojulikana kwa muda baada ya maofisa mikopo kumfuatilia nyumbani kuulizia kulikoni harejeshi mkopo aliochukulia.
“Nilishtukia watu wanakuja kubisha hodi nyumbani kwangu. Nilipotaka kujua kulikoni wakaniambia wanamtaka mkamwana wangu kwani hajarudisha mkopo. Nami nikashangaa na kuwauliza, mkopo gani huo?
“Wakanijibu kuwa alichukua mkopo wa Vicoba lakini hajarudisha. Ndipo nikawaambia mimi sina taarifa yoyote kuhusu mkopo huo na wala hakai hapa kwani ana nyumbani kwake, hivyo wakamfuate huko huko.
“Nikawaambia kwa kuwa hakunishirikisha siwezi kusaidia chochote ila wamfuate kwake. Nao maofisa hao wakaniambia kuwa wamemfuata kwake hawajamkuta na mlango umetiwa kufuli kubwa. Kumbe kwa karibu wiki mama huyo alikuwa haonekani nyumbani pengine kukwepa kudaiwa mkopo huo”.
Mpenzi msomaji, hivyo ndivyo vituko vya mikopo. Ukichukua hela za mkopo huwa ni tamu sana. Lakini ngoja uanze kuzirejesha ndipo kazi inapoanzia. Nakubaliana na mzee John hapo juu kwamba nidhamu ni msingi muhimu kwa wale wanaokopa kwa ajili ya miradi mbalimbali.
Mikopo inatakiwa imnufaishe mkopaji kwa kupata faida. Na faida hiyo aitumie kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujianzishia miradi mingine ya maendeleo.
Mpenzi msomaji, ni ukweli kwamba mikopo ina umuhimu wake mkubwa katika kujiendesha na kujiendeleza kiuchumi. Lakini umuhimu huo unaweza kuwa hauna maana kama walengwa hawataandaliwa vema katika kuipata na pia elimu ya kuanzisha na kusimamia miradi itokanayo na mikopo hiyo na pia elimu juu ya urejeshaji wa mikopo yenyewe.
Wapo waliozingatia masharti na taratibu za uanzishwaji wa miradi mbalimbali kupitia mikopo na wakapata mafanikio makubwa. Lakini wapo pia waliodhani ni suala la masihara na pindi walipopata mikopo wakaichezea na matokeo yake wakashindwa kuirejesha.
Baadhi ndio kama hao wanaozikimbia nyumba zao kwa kushindwa kurejesha na wengine kujikuta wakinyang’anywa mali kufidia mikopo hiyo. Mikopo inahitaji umakini na nidhamu pindi unapoingia katika mikataba yake. Tuzingatie masharti ya mikopo ili itunufaishe. Au siyo msomaji wangu?
Kwa leo naishia hapa ili nawe uchangie na ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0774268581(usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com
Kumbuka kama hutapenda jina au simu yako itajwe gazetini tamka hivyo na hilo litaheshimiwa.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake