ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 2, 2013

Vitambulisho vya Taifa kutolewa wiki ijayo

Baada ya sherehe hizo za uzinduzi wa utoaji Vitambulisho vya Taifa, maofisa wa NIDA watatoa vitambulisho kwa wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar

HATIMAYE vitambulisho vya taifa vitaanza kutolewa rasmi siku saba zijazo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza.

NIDA imebainisha hayo wakati ujumbe wake ulipomtembelea Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam, kukamilisha taratibu za kitambulisho chake.

Ujumbe huo ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Maimu ulieleza kuwa kuanza kutolewa rasmi kwa vitambulisho hivyo kunatokana na kukamilika kwa utengenezaji huo.
Maimu alimwambia Rais Kikwete kuwa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo utafanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam kwa kuanza kuvigawa kwa viongozi wakuu wastaafu.“Baada ya sherehe hizo za uzinduzi wa utoaji Vitambulisho vya Taifa, maofisa wa NIDA watatoa vitambulisho kwa wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,” alisema Maimu.

Alimwarifu Rais Kikwete kwamba wanakadiria kutoa vitambulisho kwa Watanzania milioni 21, wenye umri wa zaidi ya miaka 18.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alitaka kujua namna nchi nyingine zinavyoendesha suala la Vitambulisho vya Taifa hasa namna ya kuvitoa bure kwa wananchi.
Maimu alimjibu kwamba kwa Tanzania gharama za Vitambulisho vya Taifa zitabebwa na taasisi zinazotumia habari na takwimu zilizoandaliwa na NIDA.
Mwananchi.

Kauli hiyo ilionyesha kumfurahisha Rais Kikwete ambaye alisema: “Nawashukuru sana kwa kufikia hatua ya sasa. Tumeanza mbali mno na suala hilo, tangu mwaka 1968. Nafurahi sana kuwa tumefikia mahali pa kuweza kutoa Vitambulisho vya Taifa.”

NIDA ilianza zoezi la kuandikisha wananchi kwa ajili ya kutoa Vitambulisho vya Taifa mwishoni mwa mwaka 2011 baada ya kukamilisha mchakato mzima wa maandalizi.

Awali vitambulisho hivyo vilipangwa Kitambulisho cha kwanza cha Taifa kuwa kimetolewa kwa mtumishi wa umma Aprili mwaka uliopita, lakini ilipofika Novemba, 2012 Maimu licha ya kukiri mpango huo, alisema kwamba ifikapo mwaka 2014 utoaji vitambulisho hivyo utakuwa umekamilika ili viweze kutumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye Uchaguzi Mkuu, mwaka 2015.

Mkurugenzi huyto wa NIDA alitaja sababu za kuchelewa kutolewa kwa watumishi wa umma kutokana na mamlaka yake kukabiliwa na upungufu wa vifaa vinavyotumiwa kuchukua alama na vidole na picha.

Alisema kuwa mamlaka yake ilitakiwa kuingiza mfumo unaotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), pamoja na anuani za makazi unaoratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

Zoezi la uandikishaji wananchi kwa ajili ya vitambulizsho hivyo lilianza mwaka uliopita ambapo ulifanyika kwa kanda mbalimbali.

No comments: