ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 8, 2013

Wakamatwa kwa kutaka kumpindua Rais Kabila

Rais Joseph Kabila
JO’BURG, Afrika kusini
POLISI Wa Afrika Kusini wamewatia mbaroni watu 19 kwa tuhuma za kuhusika na  upangaji wa njama kwa ajili ya  kuipindua Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Taifa ya Uendeshaji Mashtaka ya Kongo  ilisema kuwa  watu hao walikuwa na lengo la kupata mafunzo maalumu ya kijeshi ili kuipindua Serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Joseph Kabila. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliongeza kuwa  hadi sasa hakuna taarifa yoyote iliyoashiria kuwepo kwa uhusiano kati ya watu hao 19 waliotiwa mbaroni na kundi la waasi la Machi 23.
Watuhumiwa hao 19 ambao hadi leo hakukuwa na taarifa kamili juu ya majina yao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo katika Mji wa  Pretoria.
Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lambert Mende alisema kuwa viongozi wa nchi hiyo walikuwa na ufahamu juu ya  harakati zilizokuwa zikiendelea nje ya nchi dhidi ya Serikali.
Watu hao 19 walitiwa mbaroni katika Mkoa wa Limpopo, Kaskazini mwa Afrika Kusini.
Awali wapiganaji wa Kundi la  M23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walisisitiza kwamba, hawataondoka katika Mji wa Goma wanaoudhibiti licha ya kutakiwa kufanya hivyo na marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Uganda.
M23  Walitoa wito wa kuachia ngazi kwa  Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo wakisisitiza kwamba, hakushinda katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kukimbia kwa vikosi vya Serikali mjini Goma baada ya kuzidiwa na mashambulio ya waasi kumeteteresha nafasi ya Rais Kabila.

Mwananchi

No comments: