Michael Wambura
Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF), na mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, Michael Wambura, ameitaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF kufuta mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu kwa sababu zoezi hilo limeendeshwa na katiba, kanuni na sheria batili na isipofanya hivyo atakwenda mahakamani kudai haki kama Mtanzania.Akizungumza jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam, Wambura alieleza kuwa ili uchaguzi huo uendelee, kamati hiyo inapaswa kutumia katiba iliyopita na si ya sasa ambayo imefanyiwa marekebisho kupitia waraka.
Katibu mkuu huyo wa zamani alisema kuwa kanuni za uchaguzi zinazotumika hivi sasa zilipitishwa Januari 7 mwaka huu na katiba inayotumika ilisajiliwa kwa msajili Januari 10 mwaka huu na kuhoji "inawezekana vipi kanuni kupitishwa kabla ya katiba?"
Wambura anapinga kuendelea kwa zoezi hilo la uchaguzi kwa kusema kwamba hakuna mkutano mkuu uliofanyika Desemba 12 mwaka jana kama Rais wa TFF, Leodegar Tenga na katibu mkuu, Angetile Osiah, walivyosaini kwenye nakala ya katiba iliyopelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Michezo Nchini.
"TFF imempotosha Msajili wa vyama kupitia ibara ya 76 ya katiba ya TFF ya kuwa mkutano mkuu ulikutana Desemba 15 mwaka jana na kufanya mabadiliko hayo huku ikijua si kweli.
"Ushauri wangu ni kusimamishwa kwa matumizi ya katiba hiyo mara moja kwani siyo halali ili kuondoa uwezekano wa kutafutwa haki kwenye mahakama za kiraia kwa sababu sheria za nchi zinaruhusu," alisema Wambura.
Alisema pia kwa mujibu wa katiba mpya wanayoitumia ibara ya 49 (4), Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi na makamu wake wanapaswa kuwa wanasheria na kumtaja, Deo Lyatto, kwamba hana taaluma hiyo kama ilivyoelezwa kwenye katiba hiyo inayotumika sasa.
Aliongeza kwa kuiita Kamati ya Rufaa iliyoteuliwa kuwa ni ya 'kidhalimu' kwa sababu ina mgongano wa kimaslahi na mmoja wa wagombea ambaye ana urafiki na mwenyekiti wa kamati hiyo, Iddi Mtiginjola na sheria inakataa hali hiyo.
Hata hivyo, Mtiginjola aliliambia gazeti hili jana kuwa amekuwa akitupiwa lawama nyingi kuhusu sakata hilo lakini yeye hajali kwavile anapaswa kusimamia sheria.
"Masuala ya kisheria hayahitaji demokrasia. Kamati yangu imetoa maamuzi kwa misingi ya kisheria. Hatuko pale kumbeba mtu wala kumuonea mtu kwa namna yoyote ile," alisema Mtiginjola.
KAYUNI NA LUGENGE
Wambura alihoji kuwa kama yeye alienguliwa kuendelea kuwa mgombea katika uchaguzi huo na wa mkoa wa Mara uliopita mwaka jana akihukumiwa kwa kosa la kusimamisha uchaguzi wa Simba mwaka 2010, mbona Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alipewa cheo hicho na hata Stanley Lugenge amepitishwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji (Njombe na Iringa) bila kuendelea kuwahukumu kwa kuifikisha FAT mahakamani mwaka 2004.
Wambura pia alihoji kama yeye alienguliwa na kamati ya uchaguzi ya Lyatto kwa kuheshimu maamuzi ya Kamati ya Rufaa iliyokuwa chini ya Jaji Mstaafu John Mkwawa, kwanini kamati hiyo haijaheshimu maamuzi yaliyompitisha Jamal Malinzi kuwa mgombea wa urais kama ilivyokuwa mwaka 2008.
"Siamini kama maamuzi haya yanayofanywa hakuna mkono wa mtu wa TFF, ndiyo maana baada ya uchaguzi wa mwaka 2008, wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi wengi waliondolewa na waliokuwa upande wao waliwateua kwenye kamati nyingine," Wambura aliongeza.
Alisema pia maamuzi ya kwenda mahakamani si kwa faida yake au familia yake bali ni kwa sababu anataka utaratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ziheshimiwe.
KAULI YA KAYUNI
Akizungumza na NIPASHE jana, Kayuni alikiri kushirikiana na Lugenge kuiburuza FAT kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) liliingilia kati na wakaamua kuondoa shauri hilo.
“Ni kweli tuliishtaki FAT lakini FIFA waliingilia kati, tukaondoa kesi yetu mahakamani. Hili suala linahusiana vipi na sakata la kuenguliwa kwa Wambura?” Alihoji Kayuni.
KANUNI ZA FIFA
Kanuni za 59 na 60 za FIFA zinakataza masuala ya soka kupelekwa mahakamani. Tatizo lolote linaloshindwa kutatuliwa na kamati za shirikisho ama chama cha soka cha nchi husika, linatakiwa kupelekwa kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
Sakata la mchezo wa soka likifikishwa ama kuingiliwa na mamlaka nyingine nje ya mamlaka za soka, FIFA hujaribu kuzipatanisha pande mbili, ikishindikana hutoa muda kwa pande hizo kumaliza tatizo na ikishindikana huifungia nchi husika kushiriki mashindano yote yaliyo chini yake.
Nchi ya Kenya iliwahi kufungiwa kushiriki michuano yote ya FIFA baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia mgogoro wa kiuongozi wa uendeshaji wa chama cha soka. Na mahakama inapoingilia kati masuala ya moja kwa moja ya soka, huchukuliwa pia ni kosa kubwa kwa mujibu wa kanuni za FIFA ambazo pia zimo katika Ibara ya 48 ya katiba ya TFF.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, Ibara ya 48(2)(a) inasema: “TFF, wajumbe wake, wachezaji, viongozi, mawakala wa wachezaji hawapaswi kupeleka mahakamani masuala ya soka. Yeyote atakayekiuka kanuni hii atafukuzwa.”
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment