ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 15, 2013

Chadema wamwaga misaada Hospitali ya Mwananyamala


Mwenyekiti wa Chadem, Freeman Mbowe.
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na wanachama mkoani Dar es Salaam,  jana waliadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kutoa misaada ya vitu mbalimbali vyenye thamani Shilingi milioni mbili kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

Wakikabidhi misaada hiyo jana kwa wagonjwa, mratibu wa ziara hiyo, Ibrahim Bashe, alisema wameamua kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa waliolazwa na kufanya usafi wa mazingira yote yanayoizunguka hospitali hiyo.


Alisema wametoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwamo vyakula, vinywaji na sabuni katika wodi za akinamama wanaojifungua, watoto na wanaume wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo.

“Moja ya sera za Chadema, ni upendo kwa umma na uzalendo kwa Taifa. Hivyo tuimechagua Siku ya Wapendanao ili kuonyesha kwa vitendo namna tunavyoupenda umma wa Watanzania na tunawafariji wagonjwa kwa kuwa katika chama chetu kila mwananchi anayo thamani bila kujali hali ya afya yake,” alisema.

Alisema wanafanya hivyo ili kuunga mkono jitihada za wabunge na madiwani wa Chadema ndani ya Manispaa ya Kinondoni kwa kuboresha huduma za afya za wananchi wa ngazi zote.
“Wabunge na madiwani wetu wamekuwa wakipiga kelele ukosefu wa vitanda, upungufu wa watumishi na ubora wa huduma katika hospitali na zahanati zilizopo ndani ya Manispaa ya Kinondoni hususan Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.

AliSEMA wanatarajia kufanya hivyo katika Hospitali za Temeke, Amana na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Ngonyani Sophinias, aliwashukuru wanachama na viongozi wa Chadema kwa zoezi la kufanya usafi pamoja na utoaji wa misaada kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali yake.

“Nawashukuru wanachama hawa kwa kitendo walichokifanya huu ni mfano bora wa kuigwa na wengine, kwani licha ya changamoto nyingi zilizopo katika hospitali yangu, lakini kuiachia serikali pekee haitoshi," alisema Dk. Sophinias.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: