KUONDOLEWA KIZAZI
Yatima huyo alisema akiwa kwenye danguro hilo, baada ya kutumikishwa kingono, aliumwa na kupelekwa kwa daktari aliyebaini kuwa kizazi chake kimeharibika, hivyo kiliondolewa.
Hata hivyo, alisema hakuwahi kumuona msichana ndani ya jengo hilo akiwa analalamika kuwa na mimba, na kwamba anahisi kuwepo uwezekano kwamba walitolewa kizazi kama yeye.
KUGUNDULIKA NA VVU
Alisema Februari 11, mwaka huu, akiwa polisi Oysterbay, aliamriwa kuondoka eneo hilo kwani si sehemu ya kuishi bali kufungua mashtaka.
Alikwenda kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo, baada ya kuelekezwa kuwa atapata sehemu ya kulala.
“Usiku wa siku hiyo, nilizidiwa na asubuhi nilikwenda zahanati ya Mwenge nilikotibiwa na kuelezwa kuwa nimeambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU),”alisema.
KULAWITIWA NA POLISI
Wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Abia ukiendelea (kwa mujibu wa polisi), inadaiwa askari polisi mmoja wa kituo cha Oysterbay, manispaa ya Kinondoni binti huyo alimlawiti kwenye migomba iliyopo mita chache kituoni hapo.
Alisema polisi huyo alimfuata akiwa amelala karibu na eneo la maegesho ya magari na kumtaka waende kula chakula cha usiku.
“Baada ya chakula wakati tunarudi kwenye maegesho nilipokuwa nimelala, aliniambia nimlipe chakula alichoninunulia kwa kunifanyia tendo hilo, nilikataa lakini akanishika kwa nguvu na kunilawiti,” alidai.
Alisema kutokana na kitendo hicho, aliondoka kituoni hapo saa 12:00 asubuhi kwenda kutoa taarifa kituo cha luninga cha ITV, kwa vile polisi hawakumsaidia.
Baada ya kutoa malalamiko yake na kusaidiwa na wafanyakazi wa ITV alijitokeza polisi mwanamke ambaye inadaiwa alimpeleka kituo kidogo cha polisi ambacho hakifahamu.
Kisha wakaelekea kituo cha mabasi Ubungo ili kurudishwa nyumbani kwao Manyara badala ya kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Nilivyochukuliwa ITV nilikuwa natokwa damu huku nyuma, nilitegemea askari angenipeleka hospitali, lakini wamenileta hapa na wananiambia wanataka kunisafirisha kwenda kwetu, ndo nasubiri hapa,” alisema na kuongeza:
“Kuna askari amenipa Shilingi 2,000 ameniambia nikale chakula pamoja na kuoga kwenye bafu lililopo kwenye jengo la abiria, lakini kwa sababu niliwasiliana na wewe kwa simu niliyomuomba mtu hapa, nikaona tutapotezana ndio maana nimekaa hapa nikusubiri,” alisema.
Wakati mwandishi akiendelea kufanya mahojiano na binti huyo, lilifika gari la polisi lenye namba PT 2083 ambalo ubavuni liliandikwa OCD Kawe, na baadhi ya askari waliokuwepo walishuka na kumchukua.
NIPASHE ilipoelekea kituo cha polisi Oysterbay ililikuta gari hilo na wakati huo lilikuwa likimteremsha binti huyo na kumwingiza mapokezi.
MAELEZO YA KAMANDA
Kaimu Kamanda wa mkoa wa Kinondoni John Mtalimbo, alipofuatwa ofisini kwake alisema taarifa zipo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kinondoni (OCD).
Aidha, alisema kwa mujibu wa OCD msichana huyo amekuwa akitangatanga maeneo ya Buguruni na sehemu nyingine ambazo hakuzitaja.
“Naona lengo lake ni kutuchafua, kwa nini asubuhi alikuja ITV na sio kutoa taarifa kwetu kama amelawitiwa na askari wetu, anatuchafua,” alisisitiza Kamanda Mtalimbo.
Alithibitisha kuwa siku tatu zilizopita, polisi ilimtafutia tiketi ili kumrudisha kwao, lakini haikufanikiwa.
Kamanda alipoulizwa sababu za kumsafirisha binti wakati amefungua kesi ya kunyanyaswa kingono kwenye danguro, alisema ni kutokana na kukosa makazi.
Awali, Mwandishi Wetu alinasa mawasiliano ya simu ya Kamanda Mtalimbo na mtu aliyeelezwa kuwa ni OCD, akimwelekeza jinsi ya kuandika maelezo dhidi ya binti huyo.
Alisikika akisema: “inabidi tujipange, hapa watakuja waandishi wa habari, (bila kujua kama mwandishi wetu alikuwepo eneo hilo), watataka kujua kinachoendelea na kumshauri aandike kuwa walikubaliana kufanya ngono,”
Licha ya kusikia kilichozungumzwa juu ya mlalamikaji huyo alipoingia ofisi kwake na kujitambulisha na kuuliza habari za binti, kamanda Mtalimbo alimweleza kuwa hana taarifa hizo na kwamba anasubiri zitoke kwa OCD.
Akisoma maelezo ya OCD wa Kinondoni mara baada ya kuletewa, Mtalimbo alisema Februari 2, mwaka huu binti aliripoti kituoni hapo kuwa alikuwa akiishi Mwananyamala alikokuwa akifanyishwa kazi za kuuza mwili na mtuhumiwa aliyemtaja kwa jina la Abia.
Alisema baada ya polisi kupokea malalamiko hayo walikwenda Mwananyamala kuonyeshwa danguro hilo na polisi walipomkamata Abia, mlalamikaji alishindwa kumtambua.
Binti ameipinga kauli hiyo na kufafanua kuwa, alipofika kwa mtuhumiwa polisi walimuuliza Abia kama anamtambua mlalamikaji, ndipo alipojibu hapana.
Alisisitiza kuwa, polisi walimuuliza kama yeye anamtambua Abia, alikiri anamfahamu kisha binti akapelekwa kwenye gari na kumuacha mtuhumiwa wake na askari wakiwa ghorofani.
Kamanda Mtalimbo aliongeza kuwa, walifungua jalada la uchunguzi wa kesi hiyo na kwa sasa mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana.
Alisema Sara aliendelea kubaki kituoni hapo hadi alipoonekana ITV Alhamis iliyopita.
Kamanda alielezwa kuwa katika mahojiano ya binti na OCD, alimfahamisha kuwa usiku wa kuamkia siku hiyo akiwa Oysterbay polisi alitongozwa na askari aliyemuahidi kumpatia Shilingi 10,000 baada ya kumlawiti.
“Walikwenda kwa makubaliano migombani na baada ya kufanya kitendo hicho, askari alimpa Shilingi 20,000 ,” alisema na kuhoji sababu za msichana huyo kutofikisha tukio hilo kituoni badala yake alikimbilia ITV.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo mlalamikaji amemtambua askari huyo kupitia gwaride la utambuzi na iwapo alichukuliwa hatua alisema bado na kuongeza:”Maelezo niliyokupa ndio ukaandike leo, mambo mengine yatafuata baadaye,”
Alipoulizwa baada ya kutoa maelezo yake kwa OCD kabla ya kuyasaini kama alisomewa ili kuyathibitisha Sara alisema hakusomewa zaidi ya kutakiwa kuweka dole gumba, kwa sababu hajui kusoma wala kuandika.
Alisema baada ya kuhojiwa na OCD, alichukuliwa na gari na kupelekwa kwa mtu mwingine (hamfahamu), ambaye alimhoji kisha akachukuliwa kwenda hospitali ya Mwanyamala.
Alisema baada ya kufikishwa Mwananyamala alifanyiwa kipimo cha kuangalia kama ni mgonjwa wa akili na kushonwa eneo alilochanika alipolawitiwa na askari.
“Baada ya vipimo daktari alitoka na kuwaeleza askari kuwa, sina tatizo la ugonjwa wa akili, ndipo waliponipeleka polisi Oysterbay polisi na kuwekwa maabusu hadi asubuhi,” alisema.
Anasema kuwa akiwa mahabusu askari aliyemlawiti, alimfuata na kuzungumza naye kwa kichaga ambapo tafsiri ya maelezo hayo ni;
“Nilikupa Shilingi 20,000 bado hujaenda kwenu, badala ya kufanya uondoke…mimi nitasaidiwa na wakubwa zangu, wewe hao waandishi wa habari hawatakusaidia lolote.”
Binti lisema asubuhi (jana) alikuja askari wa kike aliyekuwa amevaa kiraia na kumchukua kwenda kwa Afisa Ustawi wa Jamii Manispaaa ya Kinondoni.
“Tulipofika alizungumza na mwanamke tuliyemkuta kwenye ofisi hizo, baada ya kumaliza, askari alinifuata na kuniambia nisiondoke hapo mpaka nipatiwe barua ya kupeleka kwa mjumbe shina Mwanyamala, askari aliondoka na kuniacha,” alisema na kuongeza:
“Wakati nakabidhiwa barua, huyo mama aliniambia, niipeleke huko alafu mjumbe atanipeleka kwa (mtuhumiwa) ili nikaishi naye hadi hapo nauli itakapopatikana, ” alisema.
Baada ya kupata barua na maelekezo kuwa anatakiwa kwenda kuishi kwa Abia, binti alisema hayupo tayari kwa kuhofia usalama wa maisha yake kwa kuwa alishamshitaki mtu huyo.
NYUMBANI KWA ABIA
Jumatano ya wiki hii, gazeti hili lilifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kukutana na binti aliyejitambulisha kuwa anafanyakazi za ndani na kueleza kuwa mwenye nyumba hakuwepo na hajui alikokwenda.
Alipoulizwa kuhusu danguro binti huyo mwenye umri unasadikiwa kuwa kati ya miaka 15 na 17, alisema hafahamu kinachoendelea kwani mwajiri wake anamkataza kutoka nje na kukutana na majirani.
Lakini akadokeza kuwa wiki hiyo walikuja polisi wakamkamata mama huyo ambaye siku iliyofuata alirudi nyumbani.
KUWEPO MADANGURO
Majirani wa mtuhumiwa pamoja na msichana wa kazi kwenye nyumba hiyo, walikataa kutoa ushirikiano kwa kuhofia wanazungumza na polisi.
Lakini Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Kata ya Makumbusho, Said Muhunzi, alisema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo kwa danguro hilo.
“Nimebaini wapo wasichana wenye umri mdogo ambao wanaonekana na majirani wakiingizwa hapo kila mara na baadhi ya watu, majirani wamethibitisha hili,” alisema.
Aliongeza kuwa, Jumatano iliyopita kikundi chake cha ulinzi shirikishi, kilifika kwenye nyumba hiyo saa 7:00 usiku na kumkuta mtuhumiwa Abia na watu wengine wakiwa nje na kuwataka waingie ndani kwa kwani haukuwa muda wa kukaa nje.
Aliongeza kuwa watu hao ni Abia, Salome, mtoto wa marehemu mumewe (ambaye alijitambulisha kwa mwandishi kama msichana wa kazi) na wanaume watatu.
Alisema katika majibizano kati ya walinzi na watu hao, kijana mmoja anayeitwa Juma (aliyetambuliwa baada ya wenzake kumtaja) aliwatishia walinzi hao kwa bastola.
Mwenyekiti huyo akimwelezea Salome, alisema uchunguzi wake umebaini Abia amekuwa akimtumia kutafuta mabinti kwa ajili ya danguro hilo.
Kufuatia tukio hilo la walinzi kutishiwa Muhunzi alisema tayari wameshafungua kesi tatu katika kituo cha polisi Minazini na kuzitaja kuwa ni kukutwa nje wakinywa pombe usiku, kutishia kwa bastola na kuzuia ulinzi usifanyike.
Alisema walifungua jalada lenye kumbukumbu RB/118/2013 na kesi hiyo ilifikishwa kituo cha polisi Oysterbay na wao kukabidhiwa kwa PC Mwesiga.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, alisema moja ya changamoto zilizopo katika eneo lake ni kuibuka kwa madanguro na baadhi ya wasichana wenye umri mdogo kujiuza kwenye baa nyakati za usiku.
Alitaja baadhi ya baa (majina tunayo ) kuwa zinaongoza kwa kuwa na wasichana wengi wanaojiuza na kwamba wanatoa elimu kupitia kamati ya Ukimwi na kufanya msako lakini tatizo ni kubwa.
Alitaja danguro maarufu liitwalo ‘kwa wahaya’ lililopo Minazini na kusema kuwa ofisi yake inawajua watuhumiwa kwa majina.
ALILIA FEDHA ZILIZOBAKI POLISI
Binti alisema kuwa wakati anaingizwa maabusu alikuwa na Shilingi 40,000 zikiwa ni Shilingi 20,000 alipewa na askari aliyemlawiti na nyingine kutoka kwa wafanyakazi wa ITV.
Alisema mmoja wa askari wa kiume aliyekuwa kaunta alimwambia kuwa, hatakiwi kuingia mahabusu na kitu chochote, hivyo kuchukua fedha hizo.
Mwanasheria wa kujitegemea, Deogratius Mwarabu, anakosoa utaratibu uliotumika kituoni hapo, ni kosa kumuweka ndani mlalamikaji.
“Labda kama mlalamikaji alipofika kituoni kutoa taarifa zake, akakuta mtuhumiwa wake au mtu mwingine ambaye alichukua RB amemuwahi, hapo atakamatwa na sheria nyingine zitaendelea, lakini kama hicho hakikuwepo mlalamikaji akawekwa ndani hilo ni kosa,” alisema.
Kuhusu fedha zilizochukuliwa na polisi, Mwarabu alisema kwa kawaida mtuhumiwa anapoingizwa maabusu, hutakiwa kuandikisha vitu alivyonavyo kwa wakati huo.
“Kama ni fedha basi askari alitakiwa amwandikie mtuhumiwa, namba zilizopo kwenye fedha hizo, ili kesi inapoenda mahakamani wakati vielelezo vinatolewa mshtakiwa ataulizwa kama anavitambua, utambuzi wake utakuwa ni namba zile alizoandikiwa kwenye noti, “ alisema.
Kuhusu Ustawi wa Jamii kumwambia msichana huyo akakae nyumbani kwa mtuhumiwa, Mwarabu alisema hilo ni kosa na kwamba walitakiwa wamtafutie sehemu salama.
Gazeti hili linaendelea kufuatilia kisa hicho.
Yeyote atayeguswa na msichana huyu akitaka kumsaidia, awasiliane na Mhariri Mtendaji wa NIPASHE Jumapili 0774 26 85 81 kwa sababu Sara hana simu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment