Menejimenti na Bodi ya Mamlaka ya Bandari (TPA) imeshikwa kigugumizi kumweka wazi mtu aliyehusika kubadilisha kipengele cha mkataba wa ujenzi wa Mtambo wa Kupakua Mafuta kwenye Meli (SPM) bandarini na kusababisha hasara ya dola za Marekani 3 milioni karibu sawa na Sh4.8 bilioni.
Kutokana na kubadilishwa kwa kipengele hicho, TPA italazimika kutoa kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kukarabati mtambo huo ambao tayari umeanza kufanya kazi miezi sita iliyopita.
Siri ya kuondolewa kwa kipengele hicho iliwekwa hadharani Januari 18 mwaka huu na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe alipofanya ziara fupi bandarini sambamba na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoba na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Kipengele hicho kinaeleza kwamba, mara baada ya mwekezaji aliyejenga mtambo huo ambaye ni Kampuni ya Leighton ya Singapore atakapokamilisha ujenzi, angeiachia TPA vifaa vya ukarabati wa mtambo huo vyenye thamani ya Sh4.8bilioni.
Lakini baada ya mwekezaji huyo kukabidhi mtambo huo ilibainika kuwa kipengele hicho kimeondolewa hivyo kulisababishia Taifa hasara.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zilieleza kwamba kukosekana kwa vifaa hivyo kutasababisha hasara na usumbufu mkubwa kwa kukwamisha shughuli za upakuaji wa mafuta kwa kiwango cha juu.
“Kama mtambo utaharibika ni wazi kuwa hakutakuwa na vipuri… Lakini kama ikilazimu hivyo TPA itaingia gharama ya kununua vipuri hivyo wakati mkataba ulieleza kuwa spea hizo zitatolewa na mkandarasi,” Kilieleza chanzo cha habari hizi.
Katika mkutano huo wa Januari 18, mwaka huu, Dk Mwakyembe alitoa siku tatu ili apatiwe majibu ya kasoro zilizojitokeza.
Mpaka sasa Menejimenti na Bodi ya TPA wamekuwa wakigoma kuzungumzia suala hilo wakisema mwenye mamlaka ya kulizungumzia ni Waziri.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe naye alikataa kuzungumzia juu ya utekelezwaji wa maagizo yake akilitaka Mwananchi Jumapili kuwasiliana na menejimenti.
Makamu Mwenyekiti wa bodi ya TPA, Julius Mamiro aligoma kueleza hali iliyopo sasa na kutaka atafutwe Mwenyekiti wake, Profesa Joseph Msambichaka.
Profesa Msambichaka alipoulizwa alisema kuwa masuala yote ya Mamlaka hiyo yanatolewa ufafanuzi wa Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande.
“Siwezi kuzungumza mpaka nipate ruhusa kutoka kwake kwa sababu hatuwezi wote kuwa wazungumzaji,” alisema Profesa Msambichaka.
Mweananchi Jumapili lilipowasiliana na Dk Mwakyembe alisema kuwa maelezo ya kina yanaweza kutolewa na Menejimenti na bosi ya TPA.
“Wakati mwingine sio vyema kuwajibia maswali watu wa TPA. Hebu watafute uwaulize wao ndiyo wana majibu sahihi” alisema Dk Mwakyembe.
Mwananchi

No comments:
Post a Comment