ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

Chadema Arusha yatangaza mgogoro tena na RC, OCD

Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, kimetangaza mgogoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Gilles Bilabaye .

Hatua hiyo inatokana na kile kinachodai walitumia lugha na kauli za matusi dhidi ya wanachama na wafuasi wa chama hicho, kwenye harakati za kuzuia maandamano yaliyoitishwa kumshinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ajiuzulu.

Akisoma tamko la chama hicho kwa waandishi wa habari jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema viongozi hao waliwaita vijana wafuasi wa Chadema kuwa ni wahuni, wavuta bangi na wanywa viroba.

Pia, wanadaiwa kuwaita wafuasi hao kuwa hawana kazi za maana, ndiyo maana wanakubali kushiriki maandamano yanayoitishwa na chama hicho.

“Tunatoa muda wa siku tatu kwa viongozi hao kutumia njia ileile ya redio za masafa mafupi Arusha na magari ya matangazo walizotumia kutoa matusi hayo, kuomba radhi kwa vijana wa Arusha,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Kanda hiyo, Amani Golugwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao wanadaiwa kutoa kauli hizo Jumamosi na Jumapili iliyopita wakiwa katika harakati za kukabiliana na tishio la maandamano yaliyotangazwa na Chadema, kabla ya kuahirishwa baada ya makubaliano kati ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema.

Wakati Magessa akisema alitimiza wajibu na majukumu yake ya kazi kuhakikisha maandamano hayo hayafanyiki, OCD aligoma kuzungumzia tuhuma dhidi yake akisema mwenye mamlaka ya suala lolote linalohusu polisi ni Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema hawezi kuzungumzia tuhuma dhidi ya OCD wake, kwa sababu hakusikiza maneno hayo yakitamkwa.

Januari 5, 2011 Chadema waliandaa maandamano kupinga uchaguzi uliomweka madarakani Meya wa Arusha, Gaudence Lyimo matokeo yake watu watatu waliuawa na polisi.

Mwananchi

No comments: