ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 29, 2013

Ijumaa Kuu tuombee amani

Leo ni Ijumaa Kuu, siku ambayo waumini wa dini ya Kikristo wanakumbuka kuteswa kwa kuwambwa msalabani Yesu Kristo, mkombozi wa Ulimwengu.
Kwa wengine huichukulia Ijumaa Kuu kama siku ya huzuni kwao, pale ambapo ama kwa kusikia au kuangalia filamu hukumbushwa mateso ya Yesu Kristo ambayo kwa mujibu wa maandiko matakatifu aliyopata kutokana na dhambi za wanadamu.
Ijumaa Kuu ni hitimisho la mfungo wa siku 40 kwa wale ambao walikuwa wameamua kufunga. Walitumia muda huo kwa sala na kumwabudu Mungu kama alivyofanya Yesu Kristo kabla ya kuteswa.
Ni imani yetu kwamba matendo ya Kimungu ambayo tulikuwa tukihimizwa katika ibada za kila wiki na katika mfungo na kipindi cha Kwaresma, tutayaendeleza hata baada ya mfungo huo kumalizika.
Siku hii inaadhimishwa wakati ambao nchi yetu imekumbwa na matukio ya hapa na pale yenye sura ya mivutano ya kidini kati ya Wakristo na Waislamu. Matukio haya kwa kiasi fulani imeitikisa amani ya nchi yetu katika sehemu mbalimbali nchini.
Pengine si vyema kuyataja waziwazi kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawakumbusha machungu wale walioguswa nayo, lakini matukio haya ni dhahiri kwamba yamesababisha viongozi wa dini kutoa matamshi makali ambayo hayakuwa kawaida kusikika katika masikio ya Watanzania.
Tamko la mwisho ni lile lililotolewa juzi na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali Pengo ambaye aliweka bayana udhaifu wa polisi katika kufuatilia matukio hayo ya uhalifu, hasa yaliyosababisha majeraha na hata vifo vya viongozi wa dini.
Hali hii ndiyo iliyotusukuma kutoa rai hii leo kwamba baada ya hayo yote, basi na tuwe na Ijumaa Kuu yenye amani na utulivu. Tukumbuke kwamba msingi wa amani tunayoizungumzia hapa, umejengwa juu ya Kristo mwenyewe ambaye vitabu vitakatifu vinamtaja kuwa Mfalme wa Amani.
Kwa kuwa Kristo alikuja ili Ulimwengu uwe na amani, basi nasi tujenge kumbukumbu ya mateso yake katika kuitangaza amani yake kwa watu wote; wale tunaoabudu nao kanisani na hata wale wasio wenzetu kwa maana ya imani zao.
Tunapaswa kubeba wajibu huu wa kutangaza amani kama dhamana tuliyopewa tukiwa viongozi, lakini bila kusahau kwamba nje ya dini na madhehebu yetu sisi ni Watanzania wenye wajibu wa kulinda amani ya nchi yetu.
Ijumaa Kuu ifungue ukurasa mpya katika maisha yetu ya kiuhusiano, watu watakapoona matendo yetu wamtukuze Kristo kwamba kweli kifo chake kilitwaa fadhaha zetu.
Wakati tukiwahimiza viongozi wa dini kuitangaza amani wakati wa ibada za Ijumaa Kuu, tunarejea katika wito ambao tuliwahi kuutoa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha wananchi wote wanakuwa salama.
Kama alivyosema Kardinali Pengo juzi, Serikali kwa kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inabeba wajibu huo wa kuhakikisha usalama kwa watu wake wote. Usalama huu siyo wakati wa sikukuu za kikanisa pekee, bali hata katika shughuli zao nyingine za kila siku.
Tunawatakia heri na sikukuu njema ya Ijumaa Kuu, iwe ya amani na Baraka kwetu sote.

No comments: