Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa katika picha ya Pamoja, muda mfupi kabla ya Iran, Syria na Korea ya Kaskazini kukaza buti na kukataa kata kata kuunga mkono kupitishwa kwa Taarifa ya Mwisho ya Mkutano wa mwisho wa Mkataba wa Biashara ya Silaha ya Biashara (ATT( , taarifa iliyokuwa na kiambatisho cha Mkataba. Ujumbe huu wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi na ulishiriki kikamilifu katika mijidala yote iliyofanyika mchana na usiku kuhakikisha kwamba maslahi ya Tanzania yalikuwa yanazingatiwa katika Mkataba huu. Moja ya Hoja kuu ya msingi iliyosimamiwa kidete na ujumbe wa Tanzania katika majadiliano hayo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba silaha ndogo na risasi zilikuwa zinaingizwa na kwenye mkataba huo. Juhudi hizo zilifanikisha kuingizwa kwa silaha ndogo na rasasi ingawa Mkataba huo haukupitishwa kama ilivyotarajiwa.
Hizi ni baadhi ya silaha ambazo zinapashwa kudhibitiwa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Silaha, Mkataba ambao licha ya kusubiriwa kwa hamu kubwa ulishindwa kupatikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya Iran, Syria na Korea ya Kaskazini, kutia ngumu na kudai kwamba Mkataba huo ambao Rais wa Mkutano wa mwisho wa Mkataba wa Kudhibiti Biashara ya Silaha ( ATT) Balozi Peter Woolcott kutaka upitishwe kwa kauli moja, haukuwa umezingatia hoja za nchi zao pamona na nchi nyingine na kwamba ulikuwa umekumbatia maslahi ya 'wakubwa' na kwa sababu hiyo walikuwa hawauungi mkono.
Na Mwandishi Maalum
Kwa mwaka wa
Saba mfululizo Jumuiya ya Kimataifa imekwama tena mwishoni mwa
wiki iliyopita kutoka na Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti Biashara ya
Silaha ( ATT)
Mkataba huo ambao
ulitarajiwa kwa hamu kubwa, kwamba safari hii ungepatikana, ulikwamishwa
katika dakika za mwisho kabla ya
kupitishwa kwake, baada ya wajumbe kutoka Iran, Syria na Korea ya Kaskazini, kwa nyakati tofauti kueleza kwamba
hawakuwa wameridhishwa na yaliyomo katika
mkataba huo ambao ulikuwa unapendekezwa upitishwe kwa kauli moja ( Consensus).
Marchi 28 ndiyo iliyokuwa imependekezwa kwamba ingekuwa siku ya mwisho ya Mkutano wa mwisho
wa Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti
Biashara ya silaha, siku ambayo ilitarajiwa pia kwamba ripoti ya mkutano huo
ikiwa na kiambatisho cha Mkataba ingepitishwa kwa kauli moja.
Hata hivyo licha ya majadiliano ya takribani wiki
mbili na ambayo yalianza Marchi 18, 2013,wajumbe
wa mkutano huo wapatao 2000 kutoka nchi 193 wakiwamo pia washiriki kutoka Asasi
zisizo za kiserikali walijikuta wakitoka
kapa baada ya nchi tatu, Iran, Syria
na Korea ya Kaskazini kutia ngumu kuupitisha kwa kauli moja Mkataba
huo hadi pale hoja zao zitakapozingatiwa.
Kwa zaidi ya mara tatu, Rais
wa mkutano huo Balozi Peter Woolcott kutoka Australia, alijikuwa
katika wakati mgumu, pale aliposhindwa kabisa kuzishawishi nchi hizo tatu
kuungana na nchi nyingine kuupitisha
mkataba huo.
Kwa ujumla nchi hizo tatu zilieleza kwa nyakati
tofauti kwamba mkataba huo ulikuwa na mapungufu kadhaa, yakiwamo yale
waliyoyataja kwamba mkataba ulikuwa
umezingatia zaidi maslahi ya “wakubwa” na
kuacha kuingiza hoja zilizotolewa
na nchi hizo na nchi nyingine.
Aidha nchi hizo pia zilieleza bayana kwamba mkataba
huo ulikuwa unazibana zaidi serikali
lakini ulikuwa hauzugumzi lolote kuhusu makundi yenye silaha na ambayo yamekuwa yakiendesha machafuko na kutishia usalama na amani wa
nchi kadhaa.
Vile vile wajumbe
wa nchi hizo tatu walieleza kwamba Mkataba huo ambao wajumbe walikuwa
wakishawishiwa waupitishe kwa kauli moja
( Consensus), haukuwa umezungumzia haki na uhuru wa watu kujiamulia mambo yao
wenyewe hususani wale ambao walikuwa bado
wakitawaliwa kwa mabavu.
Kutoka na sababu hizo na nyinginezo, nchi hizo
zilieleza bayana kwamba zisingekuwa
tayari kuunga mkono mkataba huo.
Hali iliendelea kuwa ngumu hata pale, Balozi wa Mexico
alipojaribu kuokoa jahazi kwa kutoa pendekezo
kwamba wengi wa wajumbe wa mkutano huo walikuwa wakitaka mkataba huo
upitishwe na kwamba hapajawahi kuwapo kwa tasfri ya neno consensus.
Kauli hiyo ya Mexico iliungwa mkono na nchi kadhaa, lakini haikufua dafu kwani nchi
hizo tatu ( Syria, Iran na Korea ya Kaskazini) ziliendelea kushikilia msimamo
wao kiasi cha kumfanya Rais wa Mkutano Balozi Peter Woolcott kuamua kutangaza
kwamba, licha ya kutaka Ripoti ya
Mkutano huo wa Mwisho ambayo ilikuwa na
kiambatisho cha Mkataba ipitishwe kwa kauli moja, lakini hali haikuwa hivyo baada ya wajumbe kadhaa
kutokukubali kuipitisha kwa kauli moja na kwa sababu hiyo alikuwa anatangaza
rasmi kuufunga mkutano huo.
Kama Mkataba
huo ungepitishwa na ambapo kwa kweli unaelezwa ulijaribu safari hii kuzingatia maslahi ya kila kundi, basi ungeweka utaratibu wa kimataifa wa kudhibiti
na kuratibu biashara ya silaha karibu za
aina zote.
Silaha ambazo zingeguswa na mkataba huo ni pamoja na
vifaru vya kivita, , magari ya
kivita, ndege za kivita,
helkopta za kivita, meli za kivita, mizinga na
mitambo ya kurushia mizinga hiyo,
silaha nyepesi na ndogo na risasi.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki Moon, ameelezea masikitiko yake
makubwa juu yakutopatikana kwa mkataba
huo.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, akizungumza kupitia msemaji wake, amesema amekatishwa tamaa na matokeo ya
mkutano huo ambapo wajumbe wameshindwa kukubaliana miongoni mwao katika siku ya mwisho ya mkutano huo.
“ Mkataba ulikuwa karibu kabisa kupatikana,
ninawashukuru wale wote walioshiriki katika mchakato huu bila kuchoka ,
washukuru wale ambao pia walikuwa wamekubali kuweka kando tofauti zao” akasema
Katibu Mkuu kupitia Msemaji wake.
Akaonyesha matumaini yake kwamba iko siku mkataba huo utakuja patikana na kwamba nchi wanachama wataendelea kutafuta
njia muafaka za kupatikana kwa Mkataba huo
mapema iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment