Joketi aka Kidoti |
Na Mwandishi wetu
MWANAMITINDO nyota nchini, Joketi Mwegelo, anatarajiwa kunogesha uzinduzi wa kampeni ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto kike, unaotarajiwa kufanyika keshokutwa, ambapo shughuli mbalimbali na mada zitatolewa.
Joketi, ambaye anawika katika tasnia mbalimbali nchini ikiwemo urembo, mitindo, muziki na filamu, atashiriki kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo ijulikanayo kama Okoa Mtoto wa Kike Tanzania utakaofanyika katika Kata ya Nyamongo wilayani Tarime, Mara.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyumbani Kwanza Media Group iliyoandaa kampeni hiyo, Mossy Magere, imesema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na Joketi atawasili wilayani Tarime kesho tayari kwa kushiriki na atatoa mada ya masuala ya ujasiriamali kwa washiriki wa tamasha hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa.
Mossy alisema kuwa mbali na Joketi, wasanii mbalimbali watashiriki kutoa burudani wakiwemo wasanii nyota wa bongo fleva na wale wa asili wanaotamba mkoani Mara.
'Maandalizi yote ya msingi yamekamilika na kinachosubiriwa ni muda wa uzinduzi ufike, Joketi anatarajiwa kuwasili hapa kesho tayari kwa kushiriki nasi. Atapata fursa ya kutoa mafunzo na mbinu za kimaisha kwa washiriki ambao wengi ni wanafunzi wa shule mbalimbali wilayani hapa,' alisema Mossy.
Kampeni hiyo ambayo itadumu kwa kipindi cha miezi sita, itazinduliwa rasmi keshokutwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, ambaye ameshirikishwa kwa karibu na Kampuni ya Nyumbani Kwanza.
Alisema mchakato wa uundwaji wa klabu za wapinga unyanyasaji katika shule mbalimbali za sekondari wilayani Tarime ambapo kampeni hiyo inaanzia umekamilika na wanafunzi wamevutiwa na kujiunga kwa wingi kwenye klabu hizo ambazo zitakuwa kichocheo cha kuendeleza kampeni hiyo.
Mossy aliongeza kuwa, uundwaji wa klabu hizo unalenga kukiwezesha kizazi cha sasa na kijacho kuwa mstari wa mbele kukataa vitendo vya unyanyasaji.
“Kila jambo jema huanzia ngazi za chini, kwa sasa tunaendelea kuunda klabu za wapinga unyanyasaji ambazo zitakuwa zikipewa mafunzo na mbinu mbalimbali ili kuwajenga kufahamu madhara wakiwa wangali wadogo shuleni.
No comments:
Post a Comment