ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 22, 2013

Kamati yatimuliwa kwa mapanga

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Yasinta Assey akionyesha baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi vilivyokutwa katika eneo linalodaiwa kuwa danguro linalotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo, jana. Picha na Pamela Chilongola 

Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai kuchunguza tuhuma za kuwapo kwa danguro na uuzaji wa dawa za kulevya katika  eneo la Kipawa jana ilijikuta inashindwa kutimiza malengo yake baada ya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuwatimua wajumbe huku wakiwatishia kuwadhuru kwa zana mbalimbali yakiwamo mapanga.
Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kugundua kuwa baadhi ya wanafunzi wanatoroka shuleni na kwenda kununua dawa hizo ikiwamo bangi na eneo ambalo wanafunzi wanakwenda kufanya ngono.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Wazazi katika shule hiyo, Said Magubige, alisema walikubaliana kwenda katika eneo hilo ili kuwabaini wale wanaotumia nyumba zao kuwapokea wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya ngono na biashara ya dawa za kulevya.
“Kamati yetu ilipokwenda kufuatilia, tulishangaa kuona umati wa watu wanaokaa kwenye nyumba zilizopo karibu na shule hii, wakitufukuza kwa mapanga huku wakitoa maneno ya kutishia maisha,”alisema Magubige.
Alisema baada ya kutokea hayo walitoa taarifa kwenye Kituo kidogo cha Polisi cha Stakishari lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na matokeo yake watoto wanazidi kuharibika.
Mkuu wa Sekondari hiyo, Jansinta Assey, alikiri na kusema kwamba vitendo vya uvutaji wa bangi na biashara ya ukahaba kwa wanafunzi wake vinachangiwa na askari wa Kituo kidogo cha Polisi cha Stakishari ambao alidai wanachukua rushwa kwa wauzaji hao na nyumba bubu za wageni.
Assey alisema ni kawaida ya polisi hao kwenda kwenye nyumba kunakofanyika biashara hizo na kuchukua rushwa badala ya kutatua tatizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema hajapata taarifa za hali hiyo.
”Ngoja nimtume mkuu wa  polisi wa kituo hicho ili afuatilie”alisema Minangi.
Mwananchi

No comments: