Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa
Baadhi ya viongozi wa Kamati za Bunge waliochaguliwa juzi, wamewatumia salamu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa mashirika ya umma ambayo siku zote hesabu zake haziwi safi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo Filikunjombe aliliambia Mwananchi kuwa kwa sasa atakachoweza kusema ni kwamba anawatumia salamu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa mashirika ya Umma ambao hesabu zao haziko vizuri.
“Niwatumie salamu Makatibu Wakuu na Wakurugenzi ambao hesabu zao siyo nzuri, kwa wale wanaofanya kazi yao vizuri hatutakuwa na tatizo nao,” anasema Filikunjombe.
Alisema kuwa, bila kujali itikadi za vyama watafanya kazi zao kwa nguvu na umoja kama ambavyo waliweza kumchagua Mwenyekiti wa kamati hiyo Zitto Kabwe kwa kura nyingi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Edward Lowassa amesema mtu atahukumiwa kwa kazi ambayo ameifanya.
Lowasa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Monduli alisema “Mimi kwa sasa siwezi kusema chochote ila watu wasubiri kuona nitafanya nini na mtu atahukumiwa kwa kazi ambayo ameifanya”.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Rajab Mbarouk Mohammed alisema atahakikisha anasimamia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuhakikisha matarajio ya wananchi kutoka katika kamati hiyo yanafikiwa.
Alisema hatakuwa na kitu cha kupuuzia hususan ‘madudu’ ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya halmashauri kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Sitofanya kazi peke yangu nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha kile ambacho wananchi wanategemea kutoka kwetu kinafanikiwa,” alisema Mohammed.
Mohammed ambaye ni Mbunge wa Ole, Zanzibar (CUF) alisema anashukuru kwa kuchaguliwa kwake kwani ni mara ya kwanza kamati hiyo kuongozwa na Mzanzibari hivyo atatumia nafasi hiyo kuleta mabadiliko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini Victor Mwambalasa alisema kazi iliyopo mbele yake ni kubwa na ni ngumu inayohitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha huduma ya nishati inapatikana kwa uhakika.
Alisema kamati inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni upatikanaji wa nishati, gesi na madini mengine ambayo wakati umefika sasa kuyatafutia ufumbuzi.
“Najua kazi ni nzito na ni ngumu lakini tutaishauri Serikali kuhakikisha inatekeleza yale ina yotakiwa kutekeleza kwa wakati ili kuondoa migongano ya hapa na pale” alisema Mwambalasa.
Alisema baada ya Bunge kupitisha sheria ya ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) hivyo Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) watakiwa kufanya kazi kwa pamoja.
“Kama Tanesco watashirikiana na wawekezaji wa ndani au nje kupitia mpango wa PPP, tatizo la nishati linaweza kupungua kwa kiasi fulani” alisema Mwambalasa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment