ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 29, 2013

Kiburi cha Polisi


Deputy Director of Criminal Investigations, DCP Issaya Mngulu
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu

  Wadai wahalifu siyo kondoo wakamatike kirahisi
  Wamtaka Pengo awaeleze aliko muuaji wa Padri
 Jeshi la Polisi limemjibu kwa kejeli Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kuhusu suala la kukamatwa kwa watu waliomuua Padri wa Kanisa Katoliki, Evaristus Mushi wa Parokia ya Minara Miwili kisiwani Zanzibar, likidai wahalifu siyo kondoo waliofungiwa kwenye mti.

Kutokana na hali hiyo, limemtaka Kardinali Pengo alielekeze jeshi hilo anakojua aliko mhusika wa mauaji hayo ili wakamkamate.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu, alipozungumza na NIPASHE jana.
Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi asubuhi ya Februari 18, mwaka huu akielekea kanisani kuendesha misa. Tukio lilitanguliwa na jingine la kujeruhiwa kwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa parokia ya Mpendae, Zanzibar alipokuwa akiingia nyumbani kwake.
Katika matukio yote hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani hadi sasa.
Aidha, wakati Mngulu akitoa kauli hiyo, Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Musa Ali Musa, alisema jana kuwa suala la mauaji ya Padri Mushi, liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mngulu alisema aliyefanya mauaji hayo siyo mnyama ambaye ni rahisi kumkamata, bali ni binadamu anayetumia mbinu mbalimbali kujinusuru asikamatwe.
Alisema hayo kujibu shutuma zilizotolewa na Kardinali Pengo dhidi ya jeshi hilo kwamba, kinachoendelea tangu Padri Mushi auawe kikatili ni kama mbinu za kutaka suala hilo lisahaulike au liishe hivi hivi tu bila wahusika kukamatwa.
“Pengo aelewe kwamba, mtenda kosa, ambaye ni binadamu si sawa na kondoo aliyefungwa kwenye mti, unakwenda kumchukua kirahisi,” alisema Mngulu.
Hata hivyo, alisema wanaendelea na upelelezi wa mauaji hayo na kwamba, timu maalum ya maofisa wapelelezi wa jeshi hilo wako visiwani Zanzibar kwa kazi hiyo kwa kushirikiana na askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
“Kama Kardinali Pengo anajua lolote, basi atuelekeze twende tukamkamate huyo kondoo aliyefungwa kwenye mti,” alisema Mngulu.
Alipotakiwa kueleza hadi sasa ni watu wangapi waliokwisha kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, Mngulu alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kuelezea jambo hilo na kwamba, iwapo atawataja watuhumiwa hao anaweza kuharibu upelelezi.
Naye Kamishna Musa alipoulizwa na NIPASHE jana alisema mauaji ya Padri Mushi yalifanywa na mtu mmoja na kwamba, upelelezi wa shauri hilo unaendelea.
“Tunaendelea kuhangaika, kumtafuta, tukifanikiwa tutamfikisha mahakamani,” alisema.
Hata hivyo, alisema katika upelelezi uliokwisha kufanyika, kuna watu kadhaa waliokamatwa, ambao alisema kutokana na mazingira aliyokuwapo jana hajui idadi yao.
“Mimi hata ukiniuliza wangapi nimekamata idadi yao hata siijui, kwa sababu ni kukamata, kuhoji, kukamata, kuhoji mpaka tufike pale tunapopataka,” alisema Kamishna Musa na kuongeza:
“Mimi ukiniuliza wangapi nimewakamata ndiyo nitashindwa kujua. Kwa sababu kumbuka toka tarehe ile mpaka leo kuna watu chungu nzima tumewakamata na kuwahoji na kuwaachia.
“Wengine wamekamatwa, lakini wamepelekwa mahakamani kwa makosa mengine. Wale wengine katika kupeleleza tuliwakuta na risasi, noti bandia.”
Hata hivyo, kuhusu wauaji, Kamishna Musa alisema bado hawajafikia hatua ya kuwapeleka mahakamani na kwamba, jalada la shauri lao limepelekwa kwa DPP.
“Ngoja nikuambie kitu. Faili (jalada) hilo la mauaji liko kwa DPP. Linasubiri maelekezo ya DPP. Wala hatunalo sasa hivi polisi. Polisi tumepeleleza, upelelezi tumeufikishia hapo. Lakini pahala pa kutaka kujua nini, tumempelekea DPP kupata maelekezo yake,” alisema Kamishna Musa.
Hata hivyo, alipoulizwa kama wamekwisha kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo, Kamishna Musa alisema: “mengine usiniulize, wewe jua kwamba, kuna faili liko kwa DPP.”
Alipoulizwa kwanini mengine yasiulizwe, Kamishna Musa alisema: “Ala! Sasa wewe nitakwambia kila kitu? Kila kitu kina miiko yake. Hata wewe mambo mengine utaniambia? Hunambii ati. Kwa sababu yana miiko, yana muda. Ikishakuwa tayari nitakwambia.”
Pia alipoulizwa kama idadi ya waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo haijui, Kamishna Musa alisema: “Siwezi. Kwa mantiki ya kwamba, maana yake hili suala tunakamata na kuachia. Hao wengine tumewapeleka mahakamani baada ya kuona wana makosa mengine.
“Kwa hivyo, ukiniuliza toka siku ile nyie mmekamata wangapi, sasa hapa hivi nipo ndani ya gari nitashindwa kukwambia nilikamata watu ishirini, lakini kwa kukuhakikishia ni kwamba, kukamata, kupekua ndiyo kazi tuliyokuwa tunaifanya. Kwa hivyo, kuna watu wengi sisi tumewakamata na kuwapekua na kuwahoji.”
Kamishna Musa aliongeza: “Mimi nafikiri tuachieni siku mbili tatu tutatoa taarifa tu. Hizo kelele za watu wanavyosema wewe achana nazo kwamba polisi hawafanyi kitu we achana nao. Kila mtu atasema atakavyo wakati hajui undani wa kitu.”
Alisema kuna wahalifu walioua watu nchini Marekani wamekaa miaka 18 ndiyo wakakamatwa.
Tukio la kuuawa kwa Padri Mushi mbali na matukio hayo, pia kuna utata ndani ya jamii juu ya mashambulizi na mauaji ya viongozi wengine wa dini, akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Mathayo Kachila mkoani Geita; Imamu wa Msikiti wa Mwakaje, Kitope Zanzibar, Sheikh Ali Khamis Ali, ambaye aliuawa kwa kuchomwa kisu shingoni shambani kwake.
Pia yuko Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fedhil Suleiman Soraga, ambaye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Mwaka jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Stephen Ulimboka, alitekwa, akapigwa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande akiwa haijambui.
Machi 5, mwaka huu, Mwenyekiti wa Jukwa la Wahariri Tanzania (Tef) na Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006), Absalom Kibanda, alitekwa na kutendwa kama Ulimboka, watesi wake walimtoboa jicho, kuharibu meno yake ya mbele, kukata kidole na majeraha kadhaa kichwani.
Matukio haya yote yameacha jamii katika butwaa kubwa huku polisi wakivuta miguu bila kuwatia mbaroni wahusika wa unyama huo.
POLISI WAJIPANGA PASAKA
Jeshi la Polisi limewaondoa hofu wananchi likisema limejipanga kikamilifu kuimarisha usalama wa raia na mali zao katika kipindi chote na baada ya Sikukuu ya Pasaka, inayoadhimishwa duniani kote kuanzia leo hadi Jumatatu ijayo.
“Hivyo, wananchi washerehekee sikukuu kwa amani na utulivu, pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani,” alisema Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Senso, kupitia taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana. Alisema wakati wa sikukuu hiyo, waumini wa Kikristo hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe.
Senso alisema uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu katika maeneo mbalimbali.
“Jeshi la Polisi linapenda kuwaondoa hofu wananchi na waumini wote kuwa ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote, ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu,” alisema Senso.
Aidha, aliwatahadharisha watu wote watakaokuwa wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.
Pia aliwataka wananchi kuondoa hofu na kuwapuuza watu wachache ama kikundi cha watu wanaotumia kipindi cha sikukuu kuwatia hofu kwa kusambaza meseji za vitisho kwa watu mbalimbali kwa lengo la kuvuruga amani na utulivu.
Alisema kitendo hicho ni uhalifu kama uhalifu mwingine na kuonya kuwa iwapo watu hao watabainika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Vilevile, aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe kuzingatia uhalali na matumizi katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Pia aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.
Kadhalika aliwatahadharisha wananchi watokapo kwenye makazi yao kutoacha nyumba wazi ama bila mtu na kuwataka kutoa taarifa kwa majirani zao.“Na pale wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa kwa jeshi la polisi au viongozi wao wa serikali ya mtaa, shehia, kijiji au kitongoji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa,” alisema Senso.
Kabla ya taarifa ya Senso, Jeshi la Polisi katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya, lilitangaza kujipanga kuimarisha ulinzi kwa kupeleka makachero katika nyumba zote za ibada katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka kwa lengo la kukabiliana na uhalifu utakaojitokeza.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman wameeleza mkakati huo jana wakati wakizungumza na NIPASHE iliyotaka kujua jeshi hilo limejipanga vipi kukabiliana na matukio yatakayojitokeza wakati wa sikukuu ya Pasaka.
Naye Kamanda Athuman alisema majambazi, wezi na waporaji watambue kuwa kazi hiyo wanayoifanya kwa sasa hailipi kwani Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limejipanga kukabiliana nao hivyo ni bora wakatafuta kazi nyingine ya kufanya.

ULINZI MKALI ZANZIBAR
Pia Jeshi hilo Zanzibar, limesema ibada za Pasaka zitafanyika katika mazingira ya ulinzi mkali kufuatia matukio ya viongozi wa dini kuhujumiwa ikiwamo kupigwa risasi na kumwagiwa tindikali visiwani humo.
Tamko hilo limetolewa na Kamishina wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusu hali ya usalama wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya pasaka visiwani Zanzibar.
Alisema kwamba Jeshi la Polisi limeamua kuimarisha ulinzi wakati wote wa ibada za pasaka ili kuhakikisha waumini wa kikiristo wanashiriki ibada katika mazingira ya amani na usalama pamoja na viongozi wao.
Kuhusu taarifa za kufutwa ibada za usiku za Pasaka kwa sababu za kiusalama, Kamishina Mussa, alikanusha kuwa Jeshi lake alijatoa taarifa yoyote ya kufuta ibada za usiku kama ilivyoenezwa na baadhi ya watu katika manispaa ya mji wa Zanzibar.
Hata hivyo, Askofu wa Kanisa la TAG Dikson Kaganga alisema kwamba kutokana na sababu za kiusalama kanisa lake limeamua kufuta ratiba ya usiku ya ibada ya pasaka mwaka huu.
Alisema kwamba hatua hiyo amelazimika kuchukua kutokana na matukio matatu ya viongozi wa dini kuhujumiwa, ikiwamo kupigwa risasi na pamoja na kumwagiwa tindikali.
Alisema kwamba ibada ya Ijumaa Kuu itafanyika saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana wakati ibada kuu ya Jumapili itafanyika kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana na kuwataka waumini wake kuzingatia mabadiliko ya ratiba mpya ya ibada ya kanisa hilo.
Hata hivyo, Katibu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Jimbo la Zanzibar, Nuhu Salanya, alisema kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya ratiba ya ibada ya pasaka ya kanisa hilo.
Kwa upande wake, Padiri Cosmas Shayo wa Kanisa la Romani Katoriki Zanzibar, alisema kwamba ratiba ya ibada ya kanisa hilo itaendelea kubakia kama kawaida isipokuwa Kanisa limeamua kuchukua hatua za tafadhali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar.
Alisema kwamba tangu kujitokeza kwa vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini mahudhurio ya waumini katika ibada yamekuwa makubwa tofauti na miaka ya nyuma Zanzibar.
Katika Makanisa mbali mbali Zanzibar jana askari wa Jeshi la Polisi walionekana wakiwa wameimarisha ulinzi kabla ya kuanza kwa ibada ya Pasaka leo Zanzibar.
Imeandaliwa na Muhibu Said na Thobias Mwanakatwe (Dar) na Mwinyi Sadallah (Zanzibar).
CHANZO: NIPASHE

No comments: