10,000 waliokata rufaa matokeo kidato cha IV wafeli zaidi
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitangaza kuunda timu hiyo Februari 23, mwaka huu kwa lengo la kuchunguza sababu za asilimia 60 ya wanafunzi kufanya vibaya katika matokeo ya mtihani huo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zimethibitishwa na baadhi ya maofisa, wanafunzi waliokata rufaa wamefeli zaidi na hata walioongezewa alama matokeo hayakubadilisha madaraja waliyopata awali.
Habari zinaeleza kuwa, wanafunzi waliokata rufaa Necta kutaka mitihani yao isahihishwe upya ni takribani 10,000 na kwamba baraza bado limetoa muda zaidi kwa wengine wanaotaka kukata rufaa.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Necta viliieleza NIPASHE kuwa mitihani kwa wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 na kuhitimishwa Machi 15, mwaka huu na kwamba wengi wamefeli zaidi.
“Baada ya wanafunzi kadhaa kukata rufaa, Necta iliamua kuwaita walimu waandamizi katika masomo yote na kuanza kufanya kazi ya kusahihisha mitihani hiyo upya kwa umakini, kilichowashangaza walimu hao ni kuona kiwango cha kufeli kimeongezeka,” alisema ofisa mmoja wa Necta ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa maelezo kuwa siyo msemaji wa baraza hilo.
Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya walimu walisema walioshiriki kusahihisha mitihani hiyo walisema kuwa maoni yaliyokuwa yanatolewa na baadhi ya watu kwamba matokeo mabaya ya mtihani huo yalitokana na uchakachuaji, hayakuwa ya kweli.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, akizungumza na NIPASHE jana alithibitisha kuwa mitihani ya wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 mwaka huu. Dk. Ndalichako alisema hata hivyo, hana taarifa kama matokeo ya wanafunzi hao yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefeli zaidi kwa kuwa alikuwa safarini kikazi.
“Unavyozungumza na mimi nipo Arusha na wageni, sifahamu kama baada ya kusahihishwa upya mtihani wa wanafunzi waliokata rufaa matokeo yamekuwaje, nitafahamu baada ya kurejea Dar es Salaam Jumatano wiki hii,” alisema Dk. Ndalichako ambaye hata hivyo, hakutaja idadi ya wanafunzi waliokata rufani.
Dk. Ndalichako alisema suala la kufeli zaidi wanafunzi waliokata rufaa linawezekana kutokea kwa sababu kila mwaka imekuwa ikijitokeza hali kama hiyo, hivyo ni jambo la kawaida.
Kumekuwa na mjadala kuhusiana na matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ambao umelitikisa taifa huku kukiwa na shinikizo la kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo, wajiuzulu kutokana na matokeo hayo kuwa mabaya.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitangaza kufanyika kwa maandamano ya kuwashinikiza wajiuzulu katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam jana.
Hata hivyo, Inspekta wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, juzi jioni alikutana na ujumbe wa Chadema ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, na kukubaliana kusitishwa kwa maandamano hayo.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yaliyotangazwa na Waziri Kawambwa Februari 17, mwaka huu yalionyesha kuwa watahiniwa 240,903 (asilimia 60.6) walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 (asilimia 5.16) ndiyo waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza, la pili na la tatu.
Watahiniwa 103,327 (asilimia 26.02) walipata daraja la nne ambalo halitofautiani na sifuri kwa kuwa siyo rahisi kwa mhitimu kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika vyuo.
Jumla ya watahiniwa walikuwa 456,137, wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea wakiwa 68,806.
Watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.
Timu iliyotangazwa na Waziri Mkuu Pinda kuchunguza matokeo hayo kwa wiki sita inaundwa na Mwenyekiti wake, Profesa Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Makamu Mwenyekiti, Bernadetha Mushashu ambaye ni Mbunge wa Viti Maaulm (CCM) Mkoa wa Kagera.
Mjumbe mwengine ni Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ambaye alikataa uteuzi na kusema ni sawa na kulamba matapishi yake kwa kuwa alikuwa na mgongano na serikali juu ya hoja yake binafsi kuhusu mitalaa ambayo iliporwa kiaina bungeni na serikali.
Wajumbe wengine ni Abdul Malombwa, Profesa Mwajabu Possi, Honorath Chitanda, Daima Matemu, Mahamoud Mringo na Rakeshi Rajan.
Wengine ni Peter Maduki, Mwalimu Nurdin Mohamed ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Uali cha Alharamain, Suleiman Hemed Khamis, Abdalla Hemed Mohamed Mabrouk, Jabu Makame kutoka Baraza la Elimu Zanzibar na Kizito Lawa kutoka Taasisi ya Kukuza Mitalaa.
Wakati huo huo, timu ya Pinda jana iliendelea na kazi ya kukusanya maoni katika mikoa ya Visiwani baada ya kukamilisha kazi hiyo katika mikoa tisa ya Bara. Katibu wa timu hiyo, Edwin Mgendela, aliliambia NIPASHE jana kuwa tayari wametembelea mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Manyara, Arusha, Lindi, Shinyanga, Simiyu, Mtwara na Tanga.
Mgendela alisema kuwa watu wengi walijitokeza kutoa maoni yao mbele ya timu hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment