
Maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) na kuwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yako hatarini baada ya CCM kumtupia lawama nzito Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kwamba amekiuka makubaliano hayo yaliyofikiwa mwaka 2010.
Aidha, CCM kimemtupia lawana Maalim Seif kwamba anafanya vitendo vya kuhatarisha amani visiwani humo.
Akihutubia mamia ya wanachama na mashabiki wa CCM waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika Jumba la Vigae huko Jang’ombe mjini hapa jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alidai kuwa Maalim Seif ameanza kufanya vikao vya siri vinavyotishia kuvuruga amani na umoja wa kitaifa visiwani humo.
Vuai ambaye ni kati ya wajumbe walioshiriki katika mchakato wa mazunguzmzo yalioleta upatanishi na kufikia mwafaka wa kisiasa Zanzibar, alisema kama angejua mapema dhamira ya Maalim Seif katika mazungumzo ya kundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, angekuwa radhi kujitoa katika mazungumzo ya kufikia mwafaka.
Alisema kwamba hivi karibuni Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, aliitisha kikao maalum cha vijana wa chama chake na kusema kuwa ikiwa chama chake kitawaamrisha vijana kufanya vurugu, nchi haitatawalika na ikibidi jahazi litote na kujaa maji.
“Msingi wa mazungumzo yetu katika awamu zote za kusaka maridhiano ya kisiasa yalihimiza kujengeka kwa amani, utulivu kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa,” alisema.
Vuai aliiita kauli hiyo ni ya kichochezi na kwamba haikubaliki mbele ya jamii hivyo aliwatolea wito viongozi wa kisiasa na kiserikali kuchunga ndimi zao ili kuyaenzi mazingira yaliyoleta amani, umoja na utulivu uliopo visiwani hapa.
“Kama anahitaji jahazi litote tugawane mbao ni heri akachukua mapema ubao wake na kuelekea Mtwambwe (Pemba), lakini hatuko tayari kuona amani ya Zanzibar ikichezewa na kupotezwa kwa maslahi binafsi,” alisema Vuai.
Vuai aliendelea kudai kuwa miongoni mwa mambo waliokubaliana katika mchakato wa mazungumzo ya kusaka mwafaka ni kuwaasa wanasiasa wasitoe kauli na matamshi makali yanayoweza kuibua mpasuko wa kisiasa.
Alisema kwa muda wa mwaka mmoja CCM kimekuwa hakifanyi mikutano ya hadhara kwa kuheshimu makubaliano hayo, lakini cha ajabu viongozi wa CUF wamekuwa wakiendesha mikutano yenye lengo la kuirudisha nyuma Zanzibar.
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa utata katika Muungano, Vuai alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni halali na kuwataka wanasiasa wanaopotosha jambo hilo kukaa na kutafakari kwa kina faida zitokanazo na kuwapo kwake na athari ikiwa Muungano huo utavunjika.
“Ikiwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utavunjika, nafikiri huenda hata utulivu na maelewano kati ya Unguja na Pemba nayo yanaweza kutetereka, wanaopigia debe na kulishabikia jambo hilo litokee wanahitaji kupima pepo za nyakati na ikibidi waepukwe badala ya kuwashabikia,” alisema Vuai.
Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema sera ya CCM katika Muungano ni kuendelea na mfumo wa serikali mbili na kwamba hakuna mpango wa kuwa na serikali ya mkataba au kuvunja Muungano uliopo.
NIPASHE ilimtafuta Maalim Seif jana ili kujibu madai hayo, lakini mara zote alizopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa.
Katibu wake, Issa alipoulizwa na NIPASHE jana alisema hawezi kujibu lolote kwa kuwa madai hayo yalitolewa katika jukwaa la siasa na yeye ni msaidizi wa Maalim Seif upande wa serikali.
Hivyo akashauri aulizwe Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Salim Bimani.
Baadaye, NIPASHE ilimtafuta Bimani, lakini simu yake ilikuwa imezimwa.
CHANZO: NIPASHE
3 comments:
Ni rahisi kufahamu tofauti ya mpiga debe kwa maslahi ya tumbo na mwanasiasa imara mwenye mapenzi ya kweli kwa nchi yetu ya Zanzibar.
Vuai unauhakika gani kwamba wazanzibari watapigana na kutengaana, hakuna kabisa dalili wala historia hiyo Zanzibar. Wazanzibari ni wamoja kuliko unavyofikiria wewe. Jaribu uone. Utahama wewe na familia yako Zanzibar. Wewe na Jabu ni waganga njaa tu.
Wacheni siasa za uchochezi.
Nadhani huyu bwana maalim tangu apate hiyo nafasi anatumia nguvu zake kuchafua serikali ya muungano kinyume na kazi alizoapa kufanya. Anaingiza mambo ya fujo na kushauri vijana wafanye badala ya kufanya kazi kwa bidii na kutumia opportunities zilizopo kujiendeleza, nashindwa kuelewa anafanya nini pale kama anashindwa kumsaidia rais wa Zanzibar badala yake anatengeneza majungu ili serikali ya Zanzibar ionekane dhaifu. Ni vizuri tu angeachia ngazi kwa sababu alitakiwa afanye kazi za kiutendaji, yeye anazurura tu mitaani kuelezea ubaya wa muungano na kushawishi nchi isitawalike, nadhani huyo Seif hajui wajibu wake. Jana nilisoma gazeti akiwa anazurura huko pemba kuwa kwa nini Kibaki hakwenda Zanzibar, na kumtupia lawama waziri wa mambo wa nchi za nje, lakini ameshindwa kuelewa si lazima rais anayetembelea aende ZNZ kwani ratiba ya mgeni inafanywa na ubalozi wa nchi na kuwa confirm na wizara ya nje.
Huyo maalim seif ameisha kisiasa hajui wajibu wake kama makamu wa rais AONDOKE!
Porojo tupu mrurungo wa maneno mengi kutupotezea muda hujasema hata moja la maana. Pumba tupu!
Post a Comment