ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 17, 2013

Maalim Seif Sharif Hamad azindua vilabu 15 vya uchangiaji damu

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amezindua vilabu 15 vya uchangiaji damu salama kisiwani Pemba kwa azma ya kuwahamasisha wananchi kisiwani humo kujitokeza kwa wingi kuchangia damu, ili iweze kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma hiyo.
Uzinduzi wa vilabu hivyo ambao uliambatana na Tamasha la Michezo, ulifanyika leo 17/3/2013 katika viwanja vya Ole Kianga, mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wananchi wasipuuze tabia kuchangia damu kwa sababu ni kuokoa maisha ya binaadamu na kila mtu anaweza kupata na shida ambayo itamfanya ahitaji kuchangiwa damu.
“Utaratibu wa kuchangia damu ni jambo zuri la kuokoa maisha ya watu, wananchi jitokezeni kwa wingi kuchangia benki ya damu na wala msiogope kwenda kutolewa damu”alihimiza Maalim Seif.
Aliwahimiza wafanyakazi wa serikali, wakiwemo askari wa vikosi mbali mbali vya ulinzi na usalama kujitokeza kwa wingi na kuendeleza utaratibu wa kuchangia damu salama.
Alieleza kuwa ili benki ya damu Zanzibar iweze kuwa na akiba ya kutosha na pale yanapotokea mahitaji, kama vile ajali na wakonjwa wanaohitaji kuipata bila ya taabu, wananchi wote sifa za kuchangia damu wajitokeze kwenda kuchangia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Uchangiaji damu kwa hiari Zanizbar, Dk. Mussa Magarawa alisema mwamko ulioanza kuoneshwa na baadhi ya wananchi Zanzibar kwa kujitokeza kuchangia damu umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa damu na kuokoa vifo vingi vya akinamama wajawazito na watoto wadogo.
Dk. Magarawa allisema hivi sasa Zanzibar kuna wachangiaji damu wa uhakika 8,500 ambapo wengi wao wapo kisiwani Unguja na kuna vilabu vipatavyo 75 vya wachangiaji damu.
Hata hivyo alisema msukumo mkubwa unahitajika kisiwani Pemba ambapo bado mwamko wa wananchi kujitokeza kuchangia damu ni mdogo zaidi.
Afisa Mdhamini Wizara ya Afya, Pemba, Dk. Ukasha Daudi Ukasha alisema Wizara hiyo inachukua juhudi kubwa kuhakikisha hospitali kuu kisiwani humo zinakuwa na sehemu za kuhifadhia damu na kuhakikisha huduma ya damu inakuwepo ya kutosha wakati wote.
Alisema ipo haja viongozi waunge mkono vilabu vya kuchangia damu salama na wao wenyewe wajiunge na wawe wanachama, hatua ambayo itawafanya wananchi wengi zaidi kuhamasika na kujiunga.

No comments: