ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 27, 2013

‘Mgambo Dar wachawi wa wajasiriamali’

Dar. Mbunge wa Ilala, Musa Zungu, amesema mchawi mkubwa wa maendeleo ya wajasiriamali wadogo wa Jiji la Dar es Salaam, ni mgambo wa halmashauri za manispaa.
Zungu aliyasema hayo juzi, alipokuwa akizungumza katika harambee ya kuchangia Mpango wa Kuweka na Kukoa wa Taasisi ya Poverty Fighting Tanzania.
Zaidi ya Sh80 milioni zilikusanywa katika harambee hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa PTA, wilayani Temeke.
Mbunge huyo alisema badala ya kufanya yale waliyoagizwa na waajiri wao, mgambo hao wamekuwa chanzo cha vurugu na matatizo mengi yanayowapata wafanyabiashara ndogondogo wakiwamo wanachama wa Vicoba alisema.
Alisema ingawa Serikali imeonyesha nia njema ya kurasimisha biashara ndogondogo, mgambo wamekuwa wakiongoza vitendo vya unyanyasaji na dhuluma kwa wafanyabiashara, jambo linalochangia kurudisha nyuma maendeleo yao.
Katika harambee hiyo zaidi ya vikundi 94 vya Vicoba kutoka wilayani Temeke, vilishiriki na kupata fursa ya kubadilishana mawazo pamoja na mkurugenzi wa mfuko huo ambaye pia ni Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu.
Akizungumza katika harambee hiyo, Mtemvu, aliwataka wanachama hao wa vicoba, kuhakikisha kuwa wanatumia mitaji wanayopata chini ya mpango huo, kujikwamua kiuchumi kwa kushiriki katika miradi ya maendeleo.
“Ikiwa mtatumia mitaji yenu ipasavyo, ni wazi kuwa tatizo la umaskini miongoni mwetu litapungua kama si kwisha kabisa. Kinachotakiwa ni kuwa makini katika matumizi yetu,” alisema
Alibainisha wajasiriamali wadogo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa na kwamba kwa nafasi yake, amekuwa akijitahidi kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinaondoka.
Mtemvu alianisha baadhi ya changamoto zinazowakabili wajasiriamali wadogo kuwa ni pamoja na kutokopesheka kunatokana na mitaji midogo, ukosefu wa masoko kwa ajili ya kuuza bidhaa wanazozalisha na maeneo ya kufanyia biashara.     
Mwananchi

No comments: