Advertisements

Saturday, March 2, 2013

Mkandarasi akamatwa akiiba umeme

Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limemkatia umeme Mkandarasi wa Kampuni ya Super Contruction co.LTD ambayo inafanya ujenzi wa jengo la Acacia Estates lililopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya kubainika kuiba nishati hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini baada ya kukata umeme katika jengo hilo, Mkaguzi kiongozi wa kikosi kazi cha Tanesco, Christiani Saimon, alisema kuwa mkandarasi huyo amekuwa akiwahujumu kwa kipindi kirefu.

Alisema mkandarasi huyo amejiunganishia umeme moja kwa moja kutoka kwenye nguzo ya umeme bila kupitia kwenye mita.

Saimon alisema wamekuwa wakiutumia umeme huo katika kuunganishia mashine za kukatia vyuma ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa ghorofa hizo.Alisema umeme wanaoutumia kwa ajili ya zoezi hilo ni mkubwa na ndio maana hata mita ilishindwa kuusoma na kuzimika.

Hata hivyo, Saimon alisema kinachofanyika kwa sasa ni kufuatilia kujua ni lini wameanza kuiba umeme huo kujua gharama pamoja na faini.

Alisema kikosi kazi kimejipanga kuwabaini wezi ambao wamekuwa wakilihujumu Shirika hilo pamoja na kuwachukulia hatuakukomesha vitendo hivyo.

Saimon aliwaonya wote wanashiriki vitendo hivyo vya wizi kuacha mara moja kuepuka hasara mara mbili kutokana na adhabu watakayoitoa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Mhandisi wa jengo hilo, Nyela Lameck alisema kuwa sio kweli kuwa wameanza kuiba umeme kwa muda mrefu.

“Ni leo tu ndio tumeunganisha hili Grill mashine na mwezi uliopita tulinunua umeme wa sh 150,000 ambao ulishindikana kuingia… kama kuiba ni leo tu lakini sio tumeanza muda mrefu kuiba yaani jambo dogo waandishi mmejaa utadhani sijui kuna kitu gani jamani,” alisema Mhandisi Lameck.
CHANZO: THE GUARDIAN

No comments: