Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono
Dar es Salaam. Baada ya miezi kadhaa tangu Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono aseme patachimbika ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameibuka na kusema tayari pameanza kuchimbika na amemtuhumu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi na washirika wake kuanza kuchafua jina lake.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mkono ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alisema viongozi wa jumuiya hiyo wameanza kazi ya kumchafua kwenye baadhi ya vyombo vya habari. “Mnakumbuka wakati ule nilisema patachimbika na pengine sikuwa nimeeleweka vizuri... sasa ndiyo pameanza kuchimbika,” alisema Mkono na kuongeza:
“Pataendelea kuchimbika zaidi maana haya mambo sasa ni ya kipuuzi kabisa... Inafikia mtu anaongoza kwa kuogopa kivuli cha Mkono.”
Hata hivyo, Mkono alisema katika uchaguzi mkuu wa jumuiya hiyo uliofanyika mwaka jana mjini Dodoma, alipigiwa kura nyingi ilhali jina lake halikuwa miongoni mwa wagombea.
“Mimi sikuwa mmoja wa wagombea waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, kwa sababu jina langu lilikatwa mapema lakini chakushangaza katika kura zilizopigwa kwenye uchaguzi wao, wapo wajumbe walitaka kuongozwa na Mkono,” alisema Mkono na kuongeza:
“Sasa sijui kura zangu alipewa nani na hii pekee ndiyo inawanyima usingizi...”
Alisema kuna mambo wameanza kumzushia kupitia magazeti na amepata taarifa kwamba, kuna waraka umetengenezwa maalumu kumchafua.
Mkono alisema tayari wameanza kutekeleza azma hiyo chafu kupitia magazeti, huku akiahidi kuendelea kupambana nao mpaka aone mwisho wake.
Alipoulizwa sababu ya kumhusisha moja kwa moja mwenyekiti wa Wazazi, Mkono alisema baada ya kusoma habari iliyoandikwa kwenye moja ya magazeti (siyo Mwananchi) aligundua maudhui yake yalitengenezwa na kundi linaloongozwa na mwenyekiti huyo.
Alisema baadhi ya chokochoko zinatokea sasa kwa sababu baadhi ya watu wanadhani baada ya mabadiliko ya Katiba, anaweza kugombea urais ingawa hajawai kutangaza nia ya kufanya hivyo licha ya kuwa ni haki yake.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment